TFS yakaribisha wawekezaji ufugaji nyuki

DSM; MAMLAKA ya Misitu Tanzania (TFS), iMEkaribisha wawekezaji kwenye eneo la utalii pamoja na ufugaji nyuki.

Naibu Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka TFS, Zainab Bungwa amesema hayo wakati wa upandaji miti aina ya mikoko katika ufukwe ulioko eneo la Kunduchi mkoani Dar es Salaam.

“Tunakaribisha wawekezaji waweze kuwekeza kwa ajili ya utalii. Na si utalii tu lakini wawekeze kwa ajili ya ufugaji wa nyuki.

” Misitu hii hii hutumika kwenye kuhifadhi mazingira , kwa ajili ya utalii, kutundika mizinga, kwa ajili ya wananchi kuifurahia, kupata matunda na dawa,” amesema.

Amesema pamoja na kukaribisha wawekezaji, wakala huo una mkakati wa kuwajengea uelewa vijana wa Tanzania juu ya uhifadhi wa misitu, kuwapatia utaalam na kuwapa miche ya kupanda.

“Lakini tumeendelea kupandisha hadhi misitu iwe misitu ya hifadhi ya mazingira asilia.

” Misitu ya hifadhi asilia huruhusiwi kufanya uharibifu wowote, lakini unaruhusiwa kuingia kufanya tafiti, pia kuendeleza kwa maana ya kuwekeza. Kwa hiyo mkakati wetu ni kuhakikisha nchi inakuwa ya kijani,” amesema.

Amesema mabadiliko ya tabianchi yameathiri dunia na Tanzania hivyo vijana wa Tanzania wameungana na vijana wengine kutoka nchi 24 duniani kupanda mikoko.

Naye Mwakilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Uongozi wa Vijana cha Kimataifa, Ejat Ahmed ameisema mikoko inasaidia kuchuja hewa chafu.

Amesema katika kongamano la pili la kimataifa la viongozi vijana la mabadiliko ya Tabianchi lililofanyika mkoani Dar es Salaam, limeshirikisha vijana zaidi ya 200 kutoka nchi 24 duniani.

Kwa upande wake mwanamazingira kutoka nchini Zambia, Martine Mlenga ameipongeza serikalli ya Tanzania kupitia TFS kwa jitihada zake za kuhakikisha inahifadhi mazingira.

Habari Zifananazo

Back to top button