TFS yaokoa chemchem ya maji ya moto Pwani

JITIHADA zinazofanywa na Wakala wa Misitu Tanzania ( TFS), za utunzaji wa mazingira zimewezesha kuokoa Chemchem ya Maji Moto iliyopo Rufiji mkoani Pwani ambayo joto lake lilipungua hadi kufikia nyuzi joto 45 kutoka nyuzi joto zaidi ya 100.

Ofisa Utalii wa Wilaya hiyo kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Athuman Baragaza alisema hayo hivi karibuni.

Alisema kushuka kwa joto hilo kumesababishwa na ukataji miti ovyo hali iliyosababisha eneo hilo kuwa jangwa kwani awali eneo hilo lilizungikwa na miti mingi.

Advertisement

“Kipindi hicho cha zamani watu waliweza kupika vyakula vyao hapo, walipika maboga, viazi, kuchemsha mahindi lakini baadaye uharibifu ulipokuwa mkubwa na takataka nyingi zikaletwa katika eneo hilo maji yalishuka joto na kufikia nyuzi joto 45,” alisema.

Alisema joto lilianza kupanda katika chemchem hiyo mwaka 2019 baada ya eneo hilo kukabidhiwa TFS kwa ajili ya uangalizi hivyo nyuzijoto kupanda tena na kufikia 98.

Alisema pamoja na utalii huo wa maji moto katika eneo hilo, maji hayo yamekuwa na faida nyingi katika mwili wa binadamu ndani na nje ya mwili kutokana na madini ambayo yanapatikana kwenye hayo maji.

“Maji haya yana mchanganyiko wa madini aina tatu ambayo ni calcium, chorine na sulphur.

Haya maji ukiyaoga yanasaidia kuondoa maradhi ya ngozi kama ni mtu mwenye mba, ukurutu na fangasi. Pia kwa kuyatumia ndani ya mwili yanasaidia kuondoa kukaza kwa misuli kwa hiyo watu wanaofanya mazoezi maji haya kulingana na madini yaliyopo yanasaidia,” alisema.

Pia alisema eneo hilo hutumika kwa matumizi ya kitamaduni ambapo maji hayo yanaaminika kuondoa mikosi kwa jamii inayoishi huko.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa wilaya hiyo kutoka TFS, Francis Kiondo alisema Rufiji waliadhimisha kupanda miti Aprili mosi katika eneo hilo la linalojulikana kama Kituo cha Utalii cha Kihistoria Chemchem Majimoto.

“Tumekuja kuadhimisha upandaji miti kwa lengo hasa kwa kuendelea kuhifadhi eneo hilo kwani kabla ya kuwa chini ya TFS lilikuwa limeharibika sana,” alisema.

Alisema maji katika eneo hilo yanatiririka kwa mwaka mzima kwa saa moja lita 5000 kwa saa 24 zinapatikana lita 120,000 ambazo hazipungua kuanzia Januari hadi Disemba.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *