TFS yapoteza askari sita kwa mwaka

JESHI la Uhifadhi la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu, limepoteza askari sita kwa kuuawa baada ya kushambuliwa na wananchi nyakati tofauti wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya uhifadhi.

Kamishna wa Uhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo alisema hayo jana wilayani Mvomero, mkoani Morogoro alipotembelea kituo cha hifadhi ya msitu wa Pagale ambacho kilivamiwa na watu zaidi ya 50 kwa lengo la kutaka kuwadhuru askari wa uhifadhi wa kituo hicho.

Profesa Silayo alisema matukio hayo yametokea kwa nyakati tofauti katika kipindi cha kuanzia Januari 2022 hadi Desemba 2022 katika hifadhi za kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Mashariki.

Alisema askari wa kituo cha hifadhi ya msitu wa Pagale walivamiwa na kundi la watu zaidi ya 50 kwa lengo la kutaka kuwadhuru na walipowakosa walifanya uharibifu wa mali za serikali na kuiba baadhi ya bidhaa zilizokuwa katika kituo hicho.

Kamishina wa uhifadhi wa TFS alisema, uvamizi huo ulifanyika Desemba 16, mwaka huu wakati askari walipokuwa wamekwenda kutekeleza majukumu yao na waliporejea walikuta uharibifu  mkubwa umefanyika.

Profesa Silayo alisema baada ya kutokea kwa uvamizi huo, msako mkali ulifanyika na jumla ya watuhumiwa 50 wameshakamatwa pamoja na gunia mbili na nusu za mahindi na kwa sasa  wapo chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.

Naye Mhifadhi Mkuu, Shamba la Miti la Mtibwa, wilayani Mvomero, Abdallah Mchovu alisema tukio hilo lilitekelezwa na kundi la watu hao kuanzia majira ya saa moja asubuhi hadi saa nne mchana ambapo baada ya kuwakosa askari ndio waliamua kuharibu na kuiba mali zilizokuwepo.

Mchovu alisema mali zilizoibwa ni pamoja na magunia 31 ya mahindi, viroba 10 vya unga wa ngano, kuku wa kienyeji 250, sukari kilo 25 pamoja na gunia moja la dagaa vyote hivyo vikiwa na thamani ya Sh milioni 14.

Pia alisema uharibifu mwingine ni wa mali ikiwa na kuvunjwa kwa milango na madirisha katika nyumba zote mbili zilizojengwa katika kituo hicho ambapo thamani yake inafikia Sh milioni 25.5.

Alisema katika uchunguzi wa awali umeonesha waliotekeleza uhalifu huo sio kwa wafugaji peke yao bali na wakulima ambao wana nia ya kutaka kufanya shughuli za kibinadamu katika msitu huo uliohifadhiwa kisheria.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba watuhumiwa hao wanashikiliwa ambapo wanaendelea kuwahoji ili kubaini chanzo cha tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button