PWANI: WAKALA wa Mistu Tanzania (TFS), wametoa msaada wa viwanja zaidi ya 600 vya makazi Kwa waathirika wa mafuriko Rufiji, sambamba na msaada wa Sh milioni 20 kwa ajili ya mahitaji muhimu.
Akikabidhi msaada huo Ofisa Uhusiano wa Wakala wa Mistu Tanzania (TFS), Johari Kachwamba, amesema wakala hao wameamua kutoa msaada wa fedha na makazi kwa waathirika hao kutokana na kutambua mchango mkubwa katika uhifadhi.
Amesema katika kusaidiana na serikali katika kutatua changamoto za mafuriko katika wilaya hizo wametoa msaada huo ambao wanatarajia utakwenda kutumika kama ilivyo kusudiwa.
“Tumetoka msaada huu kutokana na kutambua wananchi wa Rufiji kama wahifadhi wenzetu maana hapa Kuna Mistu 10 yenye hekta zaidi ya 32,000 hivyo fedha hizo zitasaidia katika manunuzi ya vitu muhimu bila kusahau viwanja vya makazi”amesema
Akizungumza wakati akipokea msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, amethibitisha TFS kutoa viwanja zaidi ya 600 kwa wakazi hao na kwamba tayari shughuli ya kuwagawia limeanza ambapo wametakiwa kuchangia kiasi cha Sh 10,000.