KAGERA: Wasanii wa Filamu ,viongozi wa serikali na wadau mbalimbali wa utalii zaidi ya 100 wanatarajia kufanya ziara ya kitalii inayojulikana kama The Grand Kagera Tour mkoani Kagera kwa lengo la kuibua vivutio vya utalii visivyojulikana ,ili kuongeza wigo wa utalii mkoani Kagera na kanda ya ziwa.
Mratibu wa ziara hiyo ambaye ametumia takribani miaka minne akifanya utafiti juu ya vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Kagera, Goodhope Ntiba maarufu Kama Madam Sepenga amesema kuwa utafiti wake umekamilika na jambo aliloligundua ni kuwa vivutio hivyo ni vingi lakini hakuna uwekezaji wowote uliofanyika badala yake vimeachwa hewani bila kuboreshwa hivyo Mkoa wa Kagera na taifa kwa ujumla hawanuifaki na utalii huo.
Amesema kuwa utafiti wake ulilenga zaidi namna ya kutumia vivutio vilivyopo na utamaduni wa asili ya mkazi wa mkoani hapo kukuza uchumi pale fursa inapopatikana .
“Mimi ni msanii kutoka Mkoa wa Kagera ,niliwaza kwanini nisitumie Elimu yangu na usanii wangu kujua ni kwanini Mkoa wa Kagera unapata watalii kidogo jambo kubwa ambalo nilibaini ni kuwa tunavivutio vingi sana vya kuvutia mnoo lakini hakuna anayevitambua ,hakuna aliyeviboresha,tunautalii wa utamaduni, historia za machifu,mapango ,maporomoko,mito ya uponyaji,lakini kila mmoja anapita hakuna anayetaka kujua
,Sasa The Grand Kagera Tour itaibua haya yote na baada ya hapo tunaamini viongozi na wadau wataanza kufanyia kazi “alisema Ntimba
Mjumbe wa Bodi ya waigizaji taifa, Mohamed Sekamba amesema kuwa ziara hii itatoa fursa kwa makampuni na watu wenye hotel na wananchi kwa ujumla kujiongezea kipato huku akitoa wito kwa makampuni ya usafirishaji kuchangamkia fursa ya ujio wa wageni hao wanaokuja kuutambulisha Mkoa wa Kagera katika ulimwengu wa kitalii.
Ziara ya kitalii kupitia mradi wa The Grand Kagera Tour inatarajia kufanyika February 2024 kwa kutembelea vivutio lukuki vilivyosahaulika mkoani Kagera na baada ya ziara hiyo kikao cha wadau wa utalii mkoani Kagera kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa kitajadili namna ya kuboresha na kuweka mazingira mazuri kwa vivutio hivyo ili kuvutia uwekezaji na kuchangia pato la taifa.