Tiba rekebishi maumbo, haki ya kila mhitaji

*Inaondoa sonona, tiba afya ya akili

OKTOBA 27, 2023 Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila inatarajia kufanya upasuaji wa kibingwa kupunguza uzito na kurekebisha viungo.

Upasuaji huo ni mara ya kwanza kufanyika nchini ambapo Mloganzila watashirikiana na Daktari Bingwa wa upasuaji, Muhiti Bandari.

Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Muhimbili-Mloganzila, Dk Erick Muhumba anasema upasuaji utafanyika katika tumbo kupunguza nafasi ya chakula na kuna aina tatu na ya kwanza ni kupunguza tumbo lenyewe yaani kukata sehemu ya tumbo.

Anasema aina ya pili ni kuvuka sehemu ya kuhifadhia chakula na kwenda kwenye utumbo mdogo moja kwa moja na njia ya kisasa zaidi bila kupasua sehemu ya mwili kupitia endscopia inaingia mdomoni hadi ndani ya tumbo inashonwa inakuwa na sehemu ndogo.

“Tumbo likizidi mafuta tunapunguza kama sehemu ya mwili mtu anataka kurekebisha matiti kuwa madogo au makubwa inarekebishwa na nyama za mikono kuna wengine wamejaa inaweza kurekebishwa.”

Anaongeza: “Huduma hii kwa Mloganzila gharama yake itakuwa nafuu zaidi kuliko kwenda nje ya nchi kwa hiyo tumerahisisha, watu watapata huduma kwa ukaribu na urahisi hakuna tofauti na kwenda kupata huduma nje tofauti itakuwa gharama tu.

Anaainisha kuwa gharama za upasuaji zinatofautiana kuanzia Sh milioni 15 hadi Sh milioni 22.5 ambapo inategemea na mtu na aina ya upasuaji na kadiri wanavyotofautiana na gharama zinatofautiana hata kama upasuaji ni mmoja.

Dk Muhumba anaiambia HabariLEO kuwa wanafanya upasuaji wa aina mbili ambao wa kwanza ni upasuaji wa kupunguza uzito na upasuaji rekebishi.

“Hayo ni matibabu kwa sababu kuna watu wana kisukari shida yake ni unene anapofanya upasuaji inamsaidia, lakini pia kupunguza unene inalinda, kuna magonjwa ya moyo, presha na figo na mengine yanalinda kiasi, kikubwa ni matibabu.”

Anaongeza kwa upande wa rekebishi watu wengi wanasema urembo lakini kuna watu sehemu yake ya miili yao haiwafurahishi, hajiamini na wengine wanapata sonona hivyo kurekebisha mwili ni matibabu na kuongeza makalio ni sehemu ndogo tu.

“Mfano mtu kupunguza matiti hajiamini kusimama mbele za watu na kuna wengine matiti makubwa yanaumiza mgongo wakipunguzwa yanasaidia, ni uelewa na mitazamo wenzetu huko mbele wameshaanza kufanya,” anasema Dk Muhumba.

Anasema watafanya upasuaji wa kuongeza matiti, makalio, mapaja ili kufanya mwonekano anaoupenda mhusika na kusisitiza kuwa Watanzania wengi wanatumia gharama kwenda nje ya nchi hivyo ikija hapa itasaidia.

“Bado nafasi zipo watakaojitokeza wote watapata huduma ya upasuaji huu, sasa waliokuwa wanafanyiwa nje hawataenda na hela itabaki ndani ya nchi na tutapunguza gharama za kwenda nje na tutaongeza ujuzi kwa wataalamu wetu, manufaa yako mengi.”

Faida za upasuaji huu

 Miongoni mwa faida za upasuaji huo ambazo zimeelezwa na Dk Muhumba ni pamoja na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza yanayosababishwa na uzito mkubwa ikiwemo shinikizo la juu la damu, saratani, magonjwa ya figo, magonjwa ya moyo, kiharusi na mengine.

Aidha, anasema wapo watu wanapata msongo wa mawazo kutokana na kutojikubali maumbile yao hivyo watakapofanyiwa upasuaji watajiamini na kuepukana na sonona hivyo kuwa na afya njema mambo ambayo ni mafanikio pia.

Dk Muhumba anasema Tanzania imeshaanza kufanya maandalizi kwa ajili ya utalii wa matibabu ambapo upasuaji huo wa kurekebisha maumbile ni nafasi kubwa ya utalii wa matibabu kwani watu kutoka nchi mbalimbali watakuja kufuata huduma hiyo na kuongeza kipato cha nchi.

“Watu walikuwa wanaenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata huduma za upasuaji huu wa maumbile na baada ya kuanzisha huduma ya kuweka puto tulikuwa tukiulizwa kwamba kama mtu akikonda sana na nyama kutepeta itakuwaje?

“Na watu walikuwa wanauliza sana tukaona kuna umuhimu wa kuleta mtaalamu ili huduma ije kufanyika hapa ndani ya nchi na ifanyike kwa gharama nafuu hivyo huduma hii ni muhimu katika nchi yetu,” anasisitiza.

Faida nyingine aliyoiainisha ni kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa ndani ambao watapata ujuzi wa kufanya upasuaji wa aina hiyo ili kufanyika na wataalamu wazawa wenyewe badala ya kusubiri wataalamu kutoka nje.

“Kwa hiyo tunapokuja watu wengi watapungua kwenda nje na tunaongeza uchumi katika hospitali zetu tunamshukuru kiongozi wetu Profesa Janabi (Mohammed) ‘anatusapoti’ (kutuunga mkono) sana na upasuaji huu ni wa nchi, kamati ya utalii wa matibabu iliundwa Hospitali ya Muhimbili anajitahidi kuleta huduma zinazopatikana nje,” anasema.

“Watanzania wajitokeze wale wenye uhitaji lakini vilevile hospitali iko tayari kuwahudumia huduma za nje zitakuwepo.

Wajitokeza kusajili  

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Janabi anasema watu watano wamejitokeza kujisajili ili kupata huduma ya kurekebisha maumbo huku akisema hatua hiyo inalenga matibabu.

Profesa Janabi anasema hadi sasa ni mgonjwa mmoja ameomba kufanyiwa huduma hiyo kwa ajili ya urembo ambapo awamu hii watafanya kwa watu sita hadi 10.

“Tunategemea wahitaji zaidi kwa mara ya kwanza hatuwezi kufanya wengi na muda ni mdogo tutaona, kwa sababu tutafanya nyingine na wenzetu wa Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka,” anaeleza Prof Janabi.

Utani, kejeli za mitandaoni

Katika mitandao ya kijamii watu wameibua kejeli na utani ukiwemo wa makabila kwamba sasa watu watamiminika Muhimbili-Mloganzila kurekebisha maumbo yao.

Miongoni mwa kabila lililotaniwa zaidi ni wanawake wa Kichaga ambao wanadaiwa kuwa na maumbo makubwa juu na chini wembamba. Hata hivyo, huu ni utani usioakisi ukweli wa maumbo ya wanawake wa Kichaga kwa sasa.

Mitandao mingine ya Whatsapp watu walionesha kukerwa na hatua hii wakiilaumu Hospitali ya Muhimbili kwamba imekosa kazi ya kufanya kutafuta suluhu ya magonjwa sugu kama kisukari, saratani, HIV na mengine wamegeukia kurekebisha maumbo.

Akijibu hili, Profesa Janabi alisema upasuaji wa urekebishi ni huduma ya kimatibabu kama zilivyo huduma nyingine za upasuaji au za afya hivyo ni haki ya mtu kuwa na mwonekano na afya njema hasa wenye uzito mkubwa.

Miongoni mwa urekebishi utakaofanyika ni wa watu waliowahi kupata ajali na kuharibika sura au maeneo mengine ya mwili, Muhimbili watawarekebisha na kurejea katika hali zao za awali.

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x