TIC, CRDB kushirikiana kuongeza miradi

DAR ES SALAAM: Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesaini mkataba wa makubaliano na Benki ya CRDB lengo likiwa ni kuongeza kiwango cha miradi kutoka 500 hadi 1,000.

Mkataba huo umesainiwa leo Februari 23, 2024 kwenye kituo hicho cha uwekezaji kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Gilead Teri na Afisa Biashara Mkuu wa CRDB Boma Raballa.

Katika mkataba huo CRDB itakuwa na jukumu la kufanya maboresho ya kuunda mfumo wa tathmini itakaotumiwa na watumishi wa TIC, itafunga mfumo rahisi wa malipo utakaofanywa na wawekezaji TIC, kuanzisha dirisha maalum la uwekezaji na kutoa elimu kwa umma, ikihamasisha kampeni ya kitaifa ya uwekezaji.

Afisa Biashara Mkuu wa CRDB Boma Raballa amesema lengo ni kuhakiksiha mikakati ya uwekezaji ya serikali inapewa msukumo kwa nguvu kwa ushauri wa kitaalamu na msaada mwingine muhimu utakaohitajika wa kutoa huduma hizo kwenye madawati mahususi ikiwemo dawati la kilimo biashara, madini na mafuta na gesi.

“Itasimamia utekekelezaji wa mradi huu wote tutakuwa tunatoa taarifa kwa wakati kwa wawekezaji kuhusu vivutio vilivyopo vya kuwekeza Tanzania, rasilimali na vivutio maeneo tofauti; …. “tunaamini mfumo huu utakuwa na manufaa makubwa kwa wawekezaji na umma, ubadilishaji wa fedha, mikopo na bima mbali mbali,”amesema Raballa.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Gilead Teri akizungumza amesema mwaka uliopita wamepata mafanikio makubwa kwa kiwango cha   uwekezaji kukua tofauti na mwaka 2021 na 2022.

Amesema hadi kufikia Desemba 31, 2023 walisajiliwa miradi 506 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 5.6

“Miradi hii itakapokamilika inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 200,000 kiwango hiki ni mara mbili ya miradi zaidi ya 200 iliyosajiliwa mwaka 2022 au mtaji wa takribani Dola bilioni 2 ulioingia nchini mwaka 2022, hilo ni ongezeko mara dufu,”amesema Teri.

Amesema, kwa mwaka huu Kituo hicho cha Uwekezaji  kimejiwekea lengo la kuongeza kiwango cha miradi kutoka 500 hadi 1,000.

“Tunashirikiana na CRDB ili kutimiza azma ya Rais Samia kufanya uwekezaji kuwa nguzo kuu ya kupunguza umaskini kwa watanzania,”amesema Teri

Amesema, sheria mpya ya uwekezaji ambayo Rais Samia Suluhu Hassan  aliagiza itungwe imeongeza mwamko mkubwa kwa watanzania kuwekeza, katika miezi mitatu ya kuanzia Oktoba hadi Desemba TIC ilisajili miradi 161 ukilinganisha na miradi 58 iliyosajiliwa kipindi hicho mwaka 2022 na asilimia 62 ya wawekezaji hao ni watanzania.

Amesema Tanzania inaona matunda ya kidiplomasia yanayofanywa na Rais Samia juhudi hizo takwimu zinaonyesha Januari pekee jumla ya miradi 52 imesajiliwa ikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 422. Pia miradi hiyo  inatarajiwa kutoa ajira takribani 720.

Amesema, ushirikiano walioingia na CRDB unatarajia kuwanufaisha wawekezaji wote wanaotoka nje ya nchi pamoja na wazawa.

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button