TIC yakutana na vilio vya wawekezaji Iringa

ZIARA ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo ha Uwekezaji Tanzania (TIC) imekutana na vilio vya wawekezaji mkoani Iringa ambao wengi wao wamelilalamikia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakisema sheria yake inapunguza kasi ya uwekezaji nchini.

Kutokana na TBS kulalamikiwa na wawekezaji wote waliokutana na TIC, Mwenyekiti wa Bodi ya TIC,  Dk Bilinith Mahenge ameahidi kumuagiza Mkurugenzi wa TIC kuitisha kikao cha haraka na TBS ili kwa pamoja wajadili namna changamoto zilizotajwa na wawekezaji hao zinavyoweza kufanyiwa kazi.

“Ikishindikana katika hatua hiyo, tutalifikisha suala hili kwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji kabla ya kulipeka kwa Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan,” alisema katika ziara yake alipokuwa akiwatembelea baadhi ya wawekezaji wa wadogo na wa kati wa mkoani Iringa.

Dk Mahenge alisema serikali ina utashi mkubwa wa kisiasa katika uwekezaji na kwa kuzingatia hali ya ulinzi na usalama wa nchi, fursa za kutosha na menejimenti yenye uwezo, changamoto za uwekezaji nchini zitapatiwa ufumbuzi.

“Kimsingi msingi ya uwekezaji nchini ni ya kuvutia sana na tunashukuru kiongozi wetu mkuu wa nchi ana utayari wa kupitia sheria, sera na miongozo mbalimbali ya uwekezaji. Kwahiyo tunakusanya changamoto za uwekezaji nchini na tunaamini zitamfikia,” alisema.

Katika malalamiko yao, wawekezaji hao wanailalamikia TBS kuweka ‘kwa mujibu wa sheria yake’ gharama kubwa za usajili wa bidhaa jambo linalopunguza ubunifu na kuathiri ukuaji wa sekta ya uwekezaji wa ndani.

“Kiwandani kwetu tuna uwezo wa kuzalisha zaidi ya bidhaa 50 za nyama lakini tunashindwa kufanya hivyo kwasababu TBS wanataka kila bidhaa inayozalishwa isajiliwe na usajiliwa wake ni Sh milioni 3 kwa mwaka,” alisema Steven Maruli, mwakilishi wa kiwanda cha nyama cha Mtanga cha wilayani Iringa.

Maruli alisema ili bidhaa hizo ziweze kuingia sokoni na kuuzwa katika maduka makubwa wanatakiwa kila mwaka wawe na wastani wa Sh milioni 150 za ada ya usajili wa bidhaa hizo.

“Gharama kubwa za usajili zinazuia wazalishaji wadogo na wa kati kushiriki kwenye soko. Hii inaweza kusababisha wazalishaji kusita kuzindua bidhaa mpya au kuboresha bidhaa zilizopo na hivyo kuathiri maendeleo ya sekta,” alisema.

Naye Steve Steenkamp wa Lutega Farm wilayani Iringa alisema; “TBS sio tatizo, tatizo ni ukubwa wa gharama zao. Binafsi nashindwa kumudu gharama zao ili niingie sokoni.”
Steenkamp ambaye ni mwekezaji kutoka Afrika Kusini ameyalalamikia mazingira ya uwekezaji nchini akisema pamoja na nia njema ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan yanakwamishwa na vizingiti vilivyoko katika sheria mbalimbali.

Mwekezaji huyo anayefuga ng’ombe wa maziwa na nguruwe anasema anashindwa kuziongezea thamani bidhaa zitokanazo na wanyama hao anaofuga kwasababu ya gharama za TBS.

Alisema gharama kubwa za usajili wa bidhaa zinaweza kusababisha kupungua kwa uzalishaji na athari za kiuchumi kwa Taifa hivyo ni muhimu kwa serikali na mamlaka husika kuhakikisha gharama hizo zinakuwa za busara na zinazingatia uwezo wa wazalishaji na biashara ndogo.

Kwa upande wake Meneja wa mradi wa Farm for the Future uliopo wilayani Kilolo, Osmund Ueland alisema kupunguza gharama za usajili kunaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kukuza uzalishaji na ajira.

Ueland msimamizi wa mradi huo kutoka Norway alizungumzia pia jinsi urasimu wa benki za ndani unavyokwamisha mradi wao kupata mkopo wa kuendeleza shamba hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 350.

“Mradi wetu unajishughulisha na kilimo cha mbegu za mahindi lakini pia tunalima maharege, viazi na karanga miti. Na tangu uanze mwaka 2018 tumekwishawekeza Dola Milioni 3 ambazo ni zaidi ya Sh Bilioni 7.4 za kitanzania,” alisema.

Alisema baada ya kukosa mkopo zaidi wa kuendeleza shamba hilo kutoka benki za ndani mtazamo wao kwasasa ni kupata mbia watakayeshirikiana naye kuundeleza mradi huo mkubwa wa kilimo wilayani Kilolo.

Katika kikao cha pamoja na wawekezaji wadogo na wakati kilichofanyika mjini Iringa, TIC ilielezwa wingi wa mamlaka za udhibiti kuwa ni kikwazo katika ukuaji wa sekta hiyo.

Mbali na TBS mamlaka zingine za udhibiti zilizolalamikiwa na wawekezaji hao ni pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

“Ni muimu kwa serikali na mamlaka za udhibiti kutekeleza majukumu yao kwa uwazi, haki na kwa njia inayosaidia uwekezaji na ukuaji wa uchumi. Kuna wakati hawa watu wamekuwa wakituvamia kana kwamba sisi ni wauaji,” alisema Alpha Mgimba, msambazaji wa pembejeo za kilimo mkoani Iringa

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button