TICAD-8 kuneemesha mpango wa maendeleo

BALOZI wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda ameanika maeneo ambayo Tanzania itanufaika kupitia Dola za Marekani bilioni 30 sawa na Sh trilioni 70 zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa nchi za Afrika.

Maeneo hayo ni kwenye miundombinu, nishati, maji, kilimo, mifugo, uvuvi na uchumi wa buluu.

Serikali hiyo ya Japan ilitoa fedha hizo katika Mkutano wa Nane wa Maendeleo ya Afrika (TICAD-8), uliofanyika kuanzia Agosti 27 hadi 28, mwaka huu, jijini Tunis, Tunisia.

Balozi Luvanda aliyasema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao akiwa Tokyo, Japan kuhusu mkutano huo wa TICAD-8 uliofanyika Agosti 27 hadi 28 Tunis, Tunisia.

Alisema katika mkutano huo, Tanzania iliwasilisha jumla ya miradi nane ya kipaumbele kwa mujibu wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa ajili ya kutengewa fedha na serikali ya Japan.

Aliitaja miradi hiyo itakayonufaika na fedha hizo kuwa ni mradi wa ukarabati wa barabara ya Morogoro hadi Dodoma kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 260 na mradi wa uendelezaji umwagiliaji na usimamizi wa vyanzo vya maji katika bonde la Ziwa Victoria.

Miradi mingine ni usambazaji maji wa Lugoda uliopo Mufindi, mkoani Iringa, mradi wa kuimarisha uwezo wa kufanya utafiti wa uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji, mradi wa ujenzi wa bandari nne za kisasa za uvuvi Zanzibar na uanzishaji wa maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi Zanzibar.

Aidha, mradi wa ukarabati wa Bandari ya Wete na mradi wa usafirishaji umeme wa kilovoti 400 kutoka Somanga Fungu hadi Mkuranga.

Alisema pamoja na miradi hiyo iliyowasilishwa, Tanzania imekuwa mnufaika wa mikopo nafuu inayotolewa na Serikali ya Japan chini ya jukwaa la TICAD tangu kuanzishwa kwake.

Alisema katika mkutano huo ambao Tanzania iliwakilishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, mataifa yalijadiliana namna ya kukabiliana na changamoto ili kufikia ajenda za kiuchumi.

Balozi Luvanda alisema licha ya miradi hiyo kutengeneza ajira za moja kwa moja kwa wataalamu nchini, pia Tanzania inanufaika kwa kupata ongezeko la nishati ya umeme, kupunguza kero za foleni, kupungua kwa ajali barabarani, kuongezeka kwa wataalamu nchini kutokana na fursa za mafunzo na kukua kwa kiwango cha uchumi kutokana na miradi inayotekelezwa kwenye sekta za uzalishaji.

Luvanda alisema Waziri Mkuu Majaliwa akiwa katika mkutano huo alikutana na ujumbe mbalimbali zikiwemo kampuni kubwa za uwekezaji zinazotoka kuwekeza nchini ikiwemo kampuni ya kuunganisha magari yenye nia ya kuwekeza nchini.

Aidha, alisema Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida aliahidi kusaidia sekta ya uchumi wa buluu hususani uvuvi na kujengea uwezo uvunaji wa rasilimali za bahari. Pia atasaidia Tanzania kuimarisha miundombinu ya barabara hususani za Dodoma.

Habari Zifananazo

Back to top button