Timbwili laibuka chakula cha njaa Babati

WANANCHI wa Kitongoji cha Majengo B,Kata ya Magugu wilayani Babati wamelalamikia mfumo wa uuzaji wa chakula cha njaa na kusema wahitaji hawajakipata chakula hicho bali kimeuzwa kwa wajanja.

Kilio hicho wamekitoa leo mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo akiendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya 2020/25 na kuzungumza na makundi ya jami.

Wakizungumzia kero na changamoto katika eneo hilo kwenye mkutano wa Shina wa chama hicho kitongojini hapo walimueleza Chongolo kuwa eneo hilo limekumbwa na ukame kwa muda mrefu na wananchi wanakabiliwa na njaa.

Advertisement

Wamesema waliomba kuletewa chakula na serikali cha njaa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)wakakileta lakini katika kitongoji hicho hakuna walionufaika licha ya kuandika majina kwa mtendaji wa kata.

Chongolo baada ya kusikia hayo akamtaka Mkuu wa Wilaya ya Babati Jacob Twange kutoa majibu.

Akizungumzia malalamiko hayo, Lazaro Twange amesema walipelekewa maombi ya uwepo wa njaa eneo hilo na kuyawasilisha NFRA ambao walipeleka tani 30 za mahindi ziuzwe kwa tarafa yote.

“Majina ya wahitaji kama utaratibu wa NFRA unavyoelekeza ni kwamba yanaandikwa na mtendaji kata na wenyeviti wa vitongoji wanakuwa nayo kisha wakati wa kuyauza mahindi hayo huitwa majina na kununua chakula kulingana na mahitaji yao,”amesema Twange.

Hata hivyo wananchi hao wakataa majibu hayo na kusema hakuna mwananchi wa kitongoji hicho aliyenunua mahindi hayo bali yaliuzwa kwa wafanyabiashara ambao wakawauzia wananchi kwa bei tofauti na ile elekezi ya shilingi 850 kwa kilo moja.

Baada ya majibu hayo Chongolo amemtaka Twange kukutana na wananchi wa kitongoji hicho kushughulikia kero hiyo na ikiwezekana iwepo kamati ndogo ya watu wa eneo hilo ili chakula kingine tani 30 zilizokuja tena kitakapouzwa majina ya wahitaji eneo hilo wayahakiki ili kuepusha wasiohusika kunufaika.