Timu 16 kushiriki kombe la polisi jamii Kigoma

TIMU 16 za mpira wa miguu kutoka kata  za manispaa ya Kigoma Ujiji zimeanza mtanange wa kutafuta bingwa wa manispaa hiyo katika mashindano ya polisi jamii yanayoandaliwa na Jeshi la polisi mkoani Kigoma.

Akifungua mashindano hayo yanayofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kawawa Ujiji Mjini Kigoma, Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii cha Jeshi la Polisi Mkoa Kigoma, Iddi Kiyogomo alisema kuwa dhamira kubwa ya mashindano hayo ni kufikisha ujumbe kwa jamii kutumia ulinzi shirikishi katika kushiriki kwenye masula ya ulinzi na usalama.

Iddi Kiyogomo Mkuu wa polisi jamii mkoa Kigoma akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma wakati wa uzinduzi wa mashindano ya kombe la polisi jamii Mkoa wa Kigoma

Kiyogomo alisema kuwa suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao unaanza na mwananchi mwenyewe na kwamba ili kuhakikisha ulinzi unakuwa imara wakati wote na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi zao kwa ufanisi lazima ushirikishwaji jamii ufanyike.

Alisema kuwa matukio mengine ya uhalifu na uvunifu wa amani yanayotokea kwenye jamii sambamba na vijana kuhusishwa kushiriki kwenye matukio hayo hivyo mashindano hayo yanalenga kuwakumbusha vijana na jamii nzima kwa ujumla kuzingatia ulinzi na usalama wa nchi yao.

Katika mashindano hayo yanayotarajia kutia namba April 30 mwaka huu mshindi wa kwanza anatarajia kuondoka na pesa Sh 400,000, seti ya jezi na mpira huku mshindi wa pili akiondoka na Sh 200,000 seti ya jezi na mpira na mshindi wa tatu atajipatia Sh100,000.

Akizungumzia kufanyika kwa mashindano hayo Diwani wa kata ya kitongoni Manispaa ya Kigoma Ujiji, Himidi Omari alisema kuwa yanania nzuri ya kuwakumbusha vijana nafasi yao ya kushiriki katika ulinzi wa taifa na kuachana na vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani.

                                     Himidi Omari Diwani wa kata ya Kitongoni manispaa ya Kigoma Ujiji

Omari alisema kuwa jeshi la polisi liliwaomba madiwani wote wa manispaa ya kigoma Ujiji kuhudhuria na kuhamasisha timu na vijana mbalimbali kuhudhuria mashindano hayo hivyo kwa kushirikiana na polisi wanaamini ujumbe kwenda kwa vijana kushiriki kwenye ulinzi shirikishi utafanikiwa.

Naye mlezi wa timu ya Kipampa inayoshiriki mashindano hayo, Mwaka Salehe alisema kuwa mashindano hayo kwao ni nafasi nzuri kwa vijana kuonyesha vipaji lakini pia yatawezesha ujumbe kwenda kwa vijana kuhusu masuala ya ulinzi na usalama kufika vizuri.

                                              Mwaka Salehe, mlezi wa timu ya Kipampa

Habari Zifananazo

Back to top button