TIRA, NHIF wawafunda wabunge kuhusu bima
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Wizara ya Afya na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) wametoa Semina kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Ukimwi kuhusu maswala mbalimbali ya Bima ya Afya hususan utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote.
Kwa upande wake TIRA ilijikita katika upande wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote (UHI) iliyosainiwa mwezi Novemba na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo sheria hiyo imeipa jukumu la kusimamia undeshaji wa bima hiyo.
Awali, akitoa wasilisho kwa niaba ya Kamishna, Meneja Ubora na Udhibiti Vihatarishi Zakaria Muyengi alisema kuwa TIRA ina uzoefu wa kusimamia skimu za bima ya afya kwani tayari inasimamia Kampuni Saba za Bima zinazojishughulisha na utoaji wa Bima ya Afya.
“Tayari TIRA ipo kwenye maandalizi ya kutekeleza jukumu hilo na kwa sasa imeshaunda timu inayopitia na kuandaa muundo ili kunzisha idara maalum itakayoshughulikia maswala ya UHI,”alisema.
Akijibu maswali ya wajumbe wa kamati hiyo ya Afya na Maswala ya Ukimwi Kamishna wa Bima Dk Baghayo Saqware alisema TIRA itatekeleza ipasavyo majukumu iliyokasimiwa kwa mujibu wa sheria na kwamba itatumia uzoefu iliyokua nao katika kusimamia sekta ya Bima ili kuboresha sekta ya afya nchini.