DSM; MAMLAKA ya Usimamizi wa Huduma za Bima Nchini (TIRA), imesema asilimia 15 tu ya Watanzania ndio wanatumia huduma za bima nchini kwa sasa na kusema lengo lao ni kuendela kuelimisha umuhimu wa bima ili ifikapo mwaka 2030 idadi hiyo ifike asilimia 50.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam na Naibu Kamishna wa TIRA, Khajida Said wakati wa uzinduzi wa huduma za Bima ya Takaful inayotolewa na Wakala wa bima Kampuni ya Galco.
Amesema hatua hiyo ya kuzinduliwa kwa huduma hiyo ya bima ya Takaful imekuja baada ya TIRA kutoa mwongozo wa jinsi ya kuoa huduma hiyo ambayo inafuata misingi na sharia ya Kiislamu.
Khadija amesema matumizi ya huduma za bima nchini bado yako kwa kiwango kidogo na kuwa ni asilimia 15 tu ya Watanzania wanatumia huduma hizo nchini kote, huku uelewa wa masuala ya bima ukiwa ni asilimia 36 na kusema lengo pia ni kuongeza uelewa ili ifikapo mwaka 2030 ufike asilimia 80.
Akizungumzia bima ya Takaful Khadija alisema ilizunduliwa kwa mara ya kwanza Zanzibar Julai mwaka huu na kwamba uzindizi huo ulikuwa tamanio la wengi wanaoamini kaika dini na sharia ya Kiislamu.
“Ni huduma ambayo inafuata misingi ya Dini ya Kiislam,tunaomba mawakala wa bima wasifanye udanganyifu, bima hii haina riba,”anasema Khadija.
Meneja Biashara wa Kampuni ya Wakala wa Bima ya Galco, Emmanuel Bagabu amesema wanatoa huduma zote za bima kwa kutumia Bima ya Takaful ambayo ilikuwa tamanio la watu wengi wanaoamini katika misingi ya dini ya Kiislamu.