Tisa kortini tuhuma za mauaji ya mlinzi
MWANZA: Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza na kusomewa shtaka la mauaji katika kesi namba 2665/2024.
Akisoma shtaka hilo leo Jumatatu Februari 05, 2024, mbela ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Juma Mpuya, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, George Ngemura amewataja washtakiwa hao kuwa ni Julias Joseph ‘Bwashee’ (22) mkazi wa Igoma jijini Mwanza, na Paul John ‘Doyi’ (23).
Wengine ni , Leonidas Juma (19) mkazi wa Mtaa wa Mwananchi jijini humo na Abdallah Hassan (31) maarufu kama ‘Dula’ mkazi wa Nundu jijini humo miongoni mwa wengine.
Wakili Ngemura ameiambia Mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Januari 15, 2024 Mtaa wa Mwananchi, Kata ya Mahina, wilayani Nyamagana kwa kumuua mlinzi, Yumen Elias (54) kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kukosa mamlaka kisheria ya kusikiliza shauri hilo kisha kurejeshwa rumande.
Hakimu Mpuya amehairisha kesi hiyo hadi februari 20, 2024 kwaajili ya kutajwa.