TMA yajivunia miaka miwili ya Rais Samia

MIAKA miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani nimengi yanaandikwa na mengi yanaelezwa juu ya utendaji wake katika sekta mbalimbali, hii yote ni kuhakikisha kazi inaendelea kama kauli mbiu ya serikali ya awamu ya sita inavyosema.

Katika kueleza mambo aliyoyatekeleza katika kipindi cha miaka miwili Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzani, TMA nayo inaeleza namna miaka hii miwili imekuwa ya neema kwao kwa kuongezewa vifaa muhimu na hivyo kuboresha taarifa wanazozitoa kwa wananchi ili kuboresha uchumi wa mtu mmojammoja na jamii kwa ujumla.

Advertisement

Katika taarifa yake ambayo wametoa kwa vyombo vya habari, Mamlaka hiyo imesema, uhakika ambao umekuwa ukipatikana katika tabiri mbalimbali unatokana na vifaa madhubuti ambavyo vimewekwa na serikali katika kipindi cha awamu ya sita.

Uboreshaji huo umejikita katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa mitambo na vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa, ununuzi wa Rada za hali ya hewa; utekelezaji wa mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma, kujenga uwezo kwa watumishi; kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo mkoani Kigoma; kuiwakilisha nchi kikanda na kimataifa katika masuala ya hali ya hewa; na kuboresha utoaji wa huduma kwa lengo la kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, Katika kipindi cha miaka hii miwili, Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 50 katika bajeti ya maendeleo kwa ajili ya ununuzi wa Rada za hali ya hewa, kununua vifaa vya hali ya hali ya hewa, ukarabati wa vituo vya hali ya hewa pamoja na ujenzi wa Kituo cha Hali ya Hewa cha Kanda ya Mashariki.

Kutokana na fedha hizo, mamlaka imefanikiwa kununua Rada nne (4) za hali ya hewa ambapo ufungaji wa Rada mbili (2) katika mikoa ya Kigoma na Mbeya unaendelea.

Aidha, utengenezaji wa Rada nyingine mbili unaendelea kiwandani nchini Marekani ambao mpaka sasa umefikia asilimia 63.

Kukamilika kwa Rada hizo nne (4) za hali ya hewa kutakamilisha lengo la muda mrefu la TMA kuwa na Rada saba (7) za hali ya hewa kwa nchi nzima.

Ni mengi ambayo TMA imetekeleza vizuri ikitaja dhamana walizopewa kikanda na kimataifa na kufanikiwa kuitangaza vizuri TMA na Tanzania kimataifa.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa Katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ilishiriki katika mikutano na mawasiliano mbalimbali yaliyohusisha JPC na nchi saba (7) ambazo ni Uganda, Msumbiji, Malawi, Afrika ya Kusini, Oman, Irani, na Rwanda.

Mafanikio haya yameifanya TMA kuweza kutimiza majukumu yake ya utoaji wa huduma, uratibu na udhibiti wa shughuli za hali ya hewa nchini kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019

Na mwisho Mamlaka inatoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia na kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *