TMDA yaja na ujumbe wa simu kudhibiti madhara ya dawa kwa watumiaji

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ina jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na udhibiti wa bidhaa za tumbaku.

Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022, TMDA imefanikiwa kutekeleza malengo yake ikiwemo kuanzisha mfumo wa kudhibiti madhara yatokanayo na matumizi ya dawa, chanjo na vifaa tiba kwa watumiaji.

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, anasema  ili kuimarisha upatikanaji wa taarifa hizo, mamlaka imeanzisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ADR Reporting Tool wa utoaji wa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta na kwa njia ya kutuma ujumbe mfupi kwenye simu.

Anasema kupitia mfumo huu, TMDA imepokea jumla ya taarifa 4,898 katika kipindi husika na hadi sasa kuna jumla ya taarifa 31,666 kwenye Mfumo wa Taarifa unaosimamiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ujulikanao kama Vigibase.

Hata hivyo, taarifa hizi ni za maudhi madogo ambayo hayapelekei kuondoa dawa kwenye soko.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Gaudensia Simwanza anasema taarifa hizo hutolewa kwa namba *152*00# baada ya hapo mtu hufuata maelekezo.

“Huduma hii inatolewa bure na mtu anaweza kupata muda wowote. Kwa mfano kuna dawa zinasababisha kichefuchefu, kutapika, usingizi usio wa kawaida, kupata kizunguzungu lakini haya ni madhara yanayotarajiwa kwenye dawa husika na si hatarishi kwa mtumiaji. Madhara hatarishi  ni kama vile kubabuka ngozi, kuvimba mwili, kuumwa hadi kulazwa hospitali na hata kusababisha kifo,” anasema Simwanza.

Akifafanua kuhusu mafanikio ya TMDA, Fimbo anasema wameendelea kuimarisha usajili wa bidhaa ambapo katika kipindi cha 2021/22 bidhaa 1,286 zimesajiliwa, kati yake bidhaa za dawa za binadamu na mifugo ni 933 na vifaa tiba na vitendanishi ni 353. Anasema idadi hiyo imefanya jumla ya bidhaa zilizosajiliwa hadi sasa kufikia 8,831.

Fimbo anasema wamesajili jumla ya maeneo 467 yanayojihusisha na biashara. “Maeneo 10,938 yalikaguliwa kwa mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la maeneo 92 yaliyokaguliwa ikilinganishwa na maeneo 10,846 yaliyokaguliwa mwaka 2020/21,” anasema.

Anabainisha kuwa wameweka wakaguzi katika vituo vya forodha 32 vinavyotambulika kikanuni kuruhusu kuingia na kutoka kwa bidhaa zinazodhibitiwa.

Anaeleza kuwa jumla ya vibali 15,478, dawa ni 6,002 na 9,476 vifaa tiba na vitendanishi zilitolewa sawa na ongezeko la asilimia 116 ikilinganisha na vibali 13,259 vilivyotolewa mwaka 2020/21.

Fimbo anafafanua kuwa jumla ya vibali 63,871 vya kuingiza na kusafirisha bidhaa nje ya nchi vimetolewa hadi kufikia Juni 2022.

“Hili limechangiwa na kuimarika kwa mfumo wa kielektroniki wa utoaji vibali vya kuingiza na kutoa nchini bidhaa unaomwezesha mteja kutuma maombi, kulipa na kupata kibali ndani ya masaa 24,” anasema.

UKAGUZI WA VIWANDA

Fimbo anasema viwanda 15 vya dawa ndani ya nchi vilikaguliwa ambapo viwanda viwili kati ya saba vipya vimekidhi vigezo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji.

“Hili ni ongezeko la viwanda sita sawa na asilimia 67 ikilinganishwa na viwanda tisa vilivyokaguliwa mwaka 2020/21, jumla ya viwanda vipya 21 vya vifaa tiba vilisajiliwa ikiwa ni ongezeko la viwanda 18 ikilinganishwa na viwanda vitatu vilivyosajiliwa mwaka 2020/21. Hadi Juni viwanda 17 vya dawa, 26 vya vifaa tiba na sita vya gesi tiba vimesajiliwa.

MSAKO SOKONI

Pamoja na hayo anasema mamlaka iliendesha oparesheni tatu maalumu katika mikoa 14 na maeneo 1,355 ya biashara yalikaguliwa.

“Thamani ya bidhaa zilizokamatwa kwa kutosajiliwa ilikuwa Sh milioni 353.8 na dawa na vifaa tiba vya serikali ilikuwa Sh milioni 13.03 na dawa zilizokwisha muda wa matumizi Sh milioni 28.6 na watuhumiwa kuchukuliwa hatua.

“Hata hivyo, kiasi cha bidhaa duni na bandia katika soko kimekuwa kikipungua na sasa tatizo la dawa duni na bandia liko kwa asilimia moja.

UFUATILIAJI UBORA

TMDA hufuatilia, kuondoa na kuteketeza bidhaa ambazo hazikidhi vigezo ili kuepusha bidhaa husika zisitumiwe na walaji.

Fimbo anabainisha kuwa jumla ya sampuli 215 za dawa zilifuatiliwa na kuchunguzwa ambapo matokeo ya uchunguzi yalionesha kuwa dawa zote sawa na asilimia 100 zilifaulu vipimo vya maabara.

Anafafanua kuwa upande wa vifaa tiba na vitendanishi, sampuli za matoleo 567 zilichunguzwa na sampuli 522 sawa na asilimia 92 zilikidhi vigezo.

Aidha, anasema idadi ya majaribio ya dawa yaliyoidhinishwa imeongezeka kutoka 11 mwaka 2020/21 na kufikia 34 mwaka 2021/22.

KUTEKETEZA BIDHAA

Kwa mujibu wa Fimbo uteketezaji wa bidhaa za dawa na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi ya binadamu umeongezeka kutoka tani 14,704.80 za thamani ya Sh bilioni 8.5 zilizoteketezwa mwaka 2020/21 na kufikia tani 35,547.47 za Sh bilioni 35.53 za mwaka 2021/22.

“Bidhaa hizi zinajumuisha bidhaa zilizotolewa taarifa na zile zilizokamatwa katika kaguzi mbalimbali,” anafafanua.

UDHIBITI TUMBAKU

Ili kufanikisha hilo anasema waliandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2021-26) wa Kitaifa wa Kupambana na Tumbaku pamoja na Mpango Kazi wa Miaka Mitano wa Udhibiti wa Tumbaku ambao umeanza kutekelezwa.

“Tumeweka tayari mfumo wa udhibiti wa bidhaa hizi na hadi sasa tumekwishatambua bidhaa zote za tumbaku zilizoko kwenye soko ambapo idadi yake hadi sasa ni bidhaa 51.

Aidha, anaeleza kuwa wameanzisha maabara ya upimaji wa bidhaa za tumbaku kwenye jengo lililoko Dodoma.

UCHUNGUZI WA SAMPULI  

Aidha, anasema TMDA ina maabara tatu ambazo zimejengwa jijini Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.

“Maabara ya kupima vifaa tiba ya Dar es Salaam imeimarishwa na maabara ya kupima bidhaa za tumbaku iliyoko Dodoma imewekewa mitambo ya kisasa ya upimaji wa bidhaa hizi.

Anaeleza kuwa maabara hizo zimefanya uchunguzi wa sampuli 1,808 za dawa, vifaa tiba, vitendanishi na vipukusi ambapo sampuli 1,644 zilifaulu.

Anasema kiwango cha ufaulu wa bidhaa zilizochunguzwa umeongezeka kutoka asilimia 88 mwaka 2020/21 hadi asilimia  91 mwaka 2021/22.

MKAKATI WA ELIMU

Fimbo anasema elimu imeendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mihadhara katika mikoa 23 nchini, kipindi cha televisheni cha TMDA NA JAMII, matangazo ya redioni na kupitia mitandao ya kijamii.

Anaainisha kuwa wameanzisha vilabu 55 vya masomo katika baadhi ya shule za sekondari katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Singida, Dodoma na Mtwara.

Kuhusu makusanyo anasema wameweza kukusanya Sh bilioni 39.9 ambayo ni asilimia 106 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 37.7 kwa mwaka.

“Kati ya fedha hizi, shilingi bilioni 35.3 ni makusanyo ya ndani na matumizi yalikuwa shilingi bilioni 37.04, gawio kwa serikali tumekwishatoa jumla ya shilingi bilioni 5.5.

MIKAKATI ZAIDI

Fimbo anasema kutokana na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa katika vituo vya forodha na maeneo ya biashara, mamlaka imeendelea kushikilia vyeti vya kimataifa na kuimarisha maabara zake.

Anasema wataendelea kuimarisha usimamizi wa makusanyo ya maduhuli kutoka vyanzo vya ndani na kutekeleza mkakati wa kuendeleza viwanda vinavyozalisha dawa ndani ya nchi.

“Kukamilisha ujenzi wa miradi ya matanuru ya kuteketeza bidhaa zisizofaa yatakayojengwa mikoa ya Pwani na Dodoma pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma bora kwa wateja na kutoa elimu kwa umma,” anasisitiza.

MAFANIKIO ZAIDI  

Anaeleza kuwa TMDA imeendelea kushikilia cheti cha ithibati kwa kiwango cha ISO 9001: 2015 baada ya kukidhi vigezo kufuatia kaguzi zinazofanyika kila baada ya miaka mitatu na wahakiki kutoka nje ya nchi.

Aidha, anasema wameendelea kushikilia hadhi kwa kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO prequalification) kwa kuwa na mifumo mahiri ya uchunguzi wa dawa.

“Vilevile TMDA ni taasisi iliyohakikiwa na kuweza kufikia ngazi ya tatu kati ya nne (Maturity Level 3) ya WHO ya ubora wa mifumo ya udhibiti wa dawa,” anabainisha.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button