MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imebainisha kuwa bidhaa za tumbaku zina kemikali zenye sumu zaidi ya 90 ikiwemo zinazosababisha magonjwa ya saratani.
Hayo yalibainishwa na Mtendaji Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo kwenye maonesho ya kimataifa ya wadau wa bidhaa za afya ya Afrika Mashariki yanayofahamika ‘Pharmatech East Africa’ yaliyoanza Agosti 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Fimbo alisema kwa sasa serikali imewekeza mashine za kisasa za kupimia kemikali za sumu katika bidhaa zote za tumbaku ikiwemo sigara.
Alisema kemikali hizo zinasababisha saratani ya damu, ya koo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza.
Pia, alisema bidhaa zozote za tumbaku ikiwemo sigara zinazoingizwa nchini wanazipitia na endapo wakiona zina kemikali sumu hizo wanaziondoa sokoni.
Baadhi ya kemikali sumu hizo ambazo TMDA wameziorodhesha ni pamoja na Acetaldehyde, Acetamide, Acetone, Acrolein, Acetamide, Anabasine, Arsenic, Anisidine, O-anisidine, Ammonia, Catechol, Carbon monoxide, Caffeic acid, Cobalt, Furan, Hydrogen cyanide, Lead na Mercury.
Kemikali zingine za sumu ni Nicotine, Nickel, Nitromethane, Ndela, Selenium, Quinoline, Styrene, Uranium 235 na uranium 238 na zingine nyingi.
Aidha, Fimbo alibainisha kuwa, dawa ambazo hazijasajiliwa hazipaswi kuwepo nchini na kuonya kwamba watakaokutwa na dawa hizo watachukuliwa hatua za kisheria.