TNMC kuwanoa wauguzi, wakunga Geita

BARAZA la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) limeweka kambi ya siku sita mkoani Geita kwa lengo la kutoa mafunzo ya maadili na sheria ya uuguzi na ukunga kwa wauguzi na wakunga katika halmashauri zote mkoani humo.

Ziara hiyo ya kawaida ina lengo la kutoa elimu ya maadili na sheria kwa wauguzi na wakunga ili kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia maadili, sheria, kanuni na taratibu ili jamii iweze kupata huduma bora na salama.

Akitoa mafunzo hayo katika Halmasahauri ya Nyang’wale Geita msajili wa baraza hilo, Agnes Mtawa amewapongeza wauguzi na wakunga kwa utoaji huduma bora kwa jamii, huku akibainisha kuwa takribani asilimia 60 hadi 80 ya watoa huduma za afya nchini ni wauguzi na wakunga.

Mwanasheria wa baraza, George Shilla amewataka wauguzi na wakunga kujitokeza katika vituo vilivyopangwa kwaajili ya mafunzo hayo ili kuijua vyema sheria hiyo ambayo inaiongoza taaluma ya Uuguzi na Ukunga.

Mwajuma Mutabazi, ambaye ni muuguzi mbobezi kutoka baraza hilo amesema ili kuwa muuguzi na mkunga mzuri ni vyema kuzingatia maadili ya taaluma hiyo huku ukitanguliza utu katika utoaji huduma.

Ikumbukwe kuwa, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) ni Mamlaka ya Kisheria iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010 na Kanuni zake, kwa lengo la kusimamia wanataluma na taaluma za Uuguzi na Ukunga.

Habari Zifananazo

Back to top button