TOC yataka vyama kuendesha mashindano ya Taifa

VYAMA na mashirikisho ya michezo nchini vimetakiwa kuendesha mashindano yao ya taifa, ili kuwa na uhalali wa kuchagua Kamisheni zao za Wachezaji, imeelezwa.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kamisheni ya Wachezaji uliofanyika mjini hapa leo.

Tandau amesema kuwa Kamisheni za Wachezaji zina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya mchezo husika kwani zimekuwa zikiwasilisha changamoto, matatizo na mambo mbalimbali kwa mashirikisho yao kwa ajili ya maendeleo ya mchezo.

Amesema kuwa kuna baadhi ya mashirikisho au vyama vya michezo, ambavyo vimeshindwa kabisa kuendesha mashindano ya taifa, hivyo vinashindwa kuchagua kamisheni zao za wachezaji kwani katika kipindi hicho ndio viongozi wa kamisheni wanachaguliwa.

Amesema kiongozi wa Kamisheni ya Wachezaji anatakiwa kuwemo katika Kamati ya Utendaji ya shirikisho au chama husika cha michezo, hivyo atawakilisha changamoto, matatizo na mambo mengine ya wachezaji kwa uongozi wa chama ili kupatiwa ufumbuzi.

Rais wa TOC, Gulam Rashid amesema kuwa mashirikisho mengi ya michezo nchini hayataki uwepo kwa kamisheni hiyo, kwani wanajua wachezaji watajua na kudai haki zao na mahitaji mengine muhimu.

Baadhi ya wachezaji walisema kuwa wengi wao wameshindwa kushirikishwa katika vikao vya Kamati za Utendaji, hivyo kushindwa kuwasilisha changamoto na matatizo wanayokutana nayo katika mchezo wao.

Habari Zifananazo

Back to top button