‘Toeni taarifa za viashiria vya Ebola kwa wakati’ 

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Beatrice Mutayoba,

MADAKTARI na watoa huduma za afya katika halmashauri nane za Mkoa wa Kagera, wametakiwa kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa wakati kuhusu viashiria vya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Hayo yamesemwa leo Septemba 3, 2022 na  Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Beatrice Mutayoba, wakati akifungua mafunzo ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa madaktari na watoa huduma hao.

Amesema  utoaji taarifa za magonjwa  ya mlipuko ziko chini kutokana na mwamko mdogo wa watumishi kutoa taarifa hizo na kuziingiza kwenye mfumo.

Advertisement

“Toeni taarifa na kuziingiza kwenye mfumo kwa haraka, kumekua na tabia mkoani na wilayani taarifa zinachelewa, taarifa inatolewa leo zinapita siku tano hakuna update yoyote,” amesema Dk Beatrice na kuongeza:

“Wakati mwingine kwenye vituo vya afya kuna taarifa za mgonjwa, lakini kwenye mfumo hakuna, hakikisheni mnaingiza taarifa zote kwenye mfumo kwa wakati, ” amesisitiza.

Amesema mafunzo hayo yatawasaidia kutoa mafunzo kwenye vituo vya afya, ngazi ya jamii  wakiwa watendaji, viongozi wa kata na vijiji na madereva wa bodaboda.

“Bodaboda ni wasafirishaji wa abiria, wanamtoa mtu sehemu moja kwenda nyingine, hivyo ni kundi muhimu ambalo litasaidia kufichua taarifa za watu watakaohisiwa kuwa na Ebola.

“Hata nchini Uganda Bodaboda ndio walisaidia kuwafichua wagonjwa wa Ebola kwa sababu walishapewa elimu, ikawa ni rahisi kwao kutoa taarifa,”amesema

Amesema  watoa huduma zaidi ya 90 wa ngazi ya chini watapatiwa mafunzo pamoja na kupewa simu janja zitakazosaidia kutoa taarifa kwa wakati.

Ameeleza kuwa dalili za ugonjwa wa Ebola ni homa kali, maumivu ya viungo na dalili nyingine za homa na kwamba zile za kutoka damu puani na maeneo mengine ni za mwisho.

Aidha, amewataka wananchi kuepuka misongamano, kutoshikana mikono, kunawa mikono na sabuni na maji tiririka mara kwa mara, kutoingiliana na wanyama pori, kutoshikana, kukumbatiana, kutoshika matapitishi na  majimaji yoyote ya mwili, ili kuepuka kupata maambukizi.

Naye Mganga wa Halmashauri ya Misenyi, Daniel Chochole, amesema wameanza kufanya matayarisho kwa kuwa ugonjwa huo upo getini, kwa vile Misenyi inapakana kwa karibu na Uganda.

Amesema hadi sasa hakuna mtu yeyote ambaye amehisiwa kuwa na  Ebola, hivyo kazi kubwa wanaifanya hivi sasa ni kutoa elimu ya  namna ya kujikinga na maambukizi.

Amesema pia wanatoa elimu mipakani, ili kupima wagonjwa wote wanaiongia na kutoka nchini wapimwe afya zao kuangalia kama kuna viashiria vya ugonjwa huo, sambamba na kuweka gari ya kubebea wagonjwa ili ikitokea amebainika mgonjwa awahishwe hospitali.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maabara Kuu ya Taifa, Menadi Beyanga, amesema mbali na kufunga maabara tembezi ya kuchunguza virusi vya ebola na kutoa majibu ndani ya saa mbili katika hospitali ya Kabyaire, pia  wamefunga mashine nyingine za kupima magonjwa mbalimbali, ili mgonjwa atakapofikishwa kituoni hapo apate huduma za vipimo vingine na matibabu.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *