‘Tozo zimesaidia afya, elimu, miundombinu’

Tozo zimesaidia afya, elimu, miundombinu

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amesema bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22, serikali ilitoa Sh bilioni 117 za tozo za miamala ya simu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 234 kwenye tarafa na kata ambazo hazikuwa na vituo vya afya.

Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma leo, katika mkutano na vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala ya tozo kwenye miamala ya Simu na benki ulioandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Amesema ujenzi wa kila Kituo cha Afya umegharimu Sh milioni 500 na umefanyika kwa upelekaji wa fedha kwa awamu 2, ambapo awamu ya kwanza zilipelekwa Sh milioni 250 na baadae Sh milioni 250 kukamilisha.

Advertisement

”Haijapata kutokea tangu tupate uhuru, kujengwa vituo 234 kwa wakati mmoja ndani ya mwaka mmoja wa fedha, ambapo ujenzi ulihusisha Majengo ya Wagonjwa wa Nje (OPD), maabara, Jengo la Wodi ya Wazazi, Jengo la Upasuaji na Jengo kwa ajili ya Kufulia,” amesema Bashungwa.

Amesema serikali imejenga miundombinu sambamba na ununuzi wa vifaa vya kisasa na pia imeajiri watumishi wa sekta ya afya 7,612 kwa ajili ya kwenda kutoa huduma katika vituo hivyo vya kutolea huduma bora kwa wananchi.

Bashungwa amesema katika sekta ya elimu, jumla ya Sh bilion 7 zimetolewa kusaidia ukamilishaji wa maboma 560, ili kupunguza mlundikano wa wanafunzi kwenye vyumba vya madarasa.

Amesema kuwa kwa upande wa elimu bila ada, serikali imehakikisha sera ya elimu bila ada  katika mwaka wa fedha 2022/23 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 346.

5.