TPA washinda tuzo mwajiri bora 2023

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetwaa tuzo ya mwajiri bora wa mwaka 2023 kwa taasisi za umma hapa nchini.

Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya mkurugenzi mkuu, Meneja wa Rasilimali Watu wa TPA , Said Msabimana amesema mafanikio hayo yametokana na mifumo bora ya uajili waliojiwekea.

Huu ni mwaka wa pili mfululizo kwa mamlaka hiyo kutwaa tuzo hiyo iliyoandaliwa na kusimamiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kufanyika kila mwisho wa mwaka.

Kwa mujibu wa wandaaji wa tuzo hizo, lengo la kuanzishwa kwake ni kutambua wanachama wanaofanya vizuri katika kuweka mikakati bora yenye kuthamini usimamizi wa rasimali watu na shughuli za biashara.

Mkurugenzi Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba amesema tuzo hizo zimeongeza tija, uhusiano bora mahala pa kazi, utii wa sheria na ushindani kibiashara.

Akizungumzia mchakato ulivyokuwa, Ndomba alisema kampuni shiriki ziliwasilisha madodoso mawili yaliyojazwa, moja likiwa limejazwa na uongozi au mkurugenzi mkuu au mkuu wa kitengo cha usimamizi wa rasilimali watu na dodoso jingine likiwa limejazwa na mwajiriwa wa kawaida au mwakilishi wa chama cha wafanyakazi.

Kwa mwaka huu, uzinduzi wa rasmi wa mchakato wa kutafuta mwajiri bora wa mwaka kwa mwaka 2023 uliofanyika mwezi Mei 30,2023.

Habari Zifananazo

Back to top button