MAMLAKA ya Usimaizi Bandari nchini (TPA), imesema iko katika maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, itakayosaidia utoaji wa huduma za upakiaji na kushusha mzigo.
Pia mesema kuanzia Januari mwaka 2023 itaanza ujenzi wa kituo kikubwa cha kisasa cha kupokelea mafuta katika bandari ya Dar es Salaam, hatua itakayosaidia meli kutotumia muda mrefu kushusha.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema hayo leo Dar es Salaam, wakati akizungumza na ujumbe wa Bodi ya Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), waliofika kutaka kujua mipango mbalimbali ya mamlaka hiyo katika kuboresha utoaji wa huduma.
Amesema ujenzi wa bandari ya Bagamoyo ulikuwa umefikia hatua ya kuzungumza na mwekezaji, lakini ghafla alijitoa na kwa sasa wameanza mchakato wa kutafuta mwingine.
Amesema mbali ya kutafuta mwekezaji lakini sehemu ya mradi wa ujenzi wa bandari hiyo utafanywa na mamlaka hiyo wenyewe, lengo kubwa ni kupunguza muda wa meli kusubiri kushusha mizigo.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya EABC, Anjelina Ngalula, alisema yeye pamoja na wafanyabiashara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wako tayari kutumia bandari ya Dar es Salaam katika kushusha mizigo yao, kwa kuwa malalamiko yaliyokuwepo awali yamefanyiwa kazi.