TPA yakana urasimu utoaji huduma bandarini

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema uwekezaji uliofanywa katika bandari nchini umeongeza ufanisi wa uwezo wa kupakua shehena za aina zote.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano ya TPA, mwishoni mwa wiki Dar es Salaam ilieleza kuwa hakuna urasimu katika utoaji huhuma bandarini hasa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Taarifa ilieleza kuwa kumekuwa na taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii zikidai kuna urasimu katika utoaji huduma bandarini.

“TPA inawathibitishia wateja, wadau na umma kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na serikali katika bandari umeongeza ufanisi na kumekuwa na ongezeko kubwa la kasi ya utoaji huduma hasa upakuaji wa shehena za aina zote hadi kufikia kukabidhi mizigo kwa mawakala wanaokamilishataratibu za kibandari kwa wakati,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa TPA inafanya kazi saa 24 kuhudumia shehena aina zote huku kitengo cha huduma kwa wateja na kituo cha mawasiliano ya simu vikiwa wazi muda wote ili kuhakikisha changamoto zote zinazoripotiwa na wateja na wadau zinapatiwa ufumbuzi haraka.

TPA imetoa rai kwa wateja wenye changamoto zozote wawasiliane na kurugenzi hiyo kwa namba za miito ya simu 0800-110032, au kutembelea kurasa za mitandao ya kijamii ya TPA ili hatua zichukuliwe mara moja.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa alisema Mbossa alisema hivi sasa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa bandari zilizopo na ujenzi wa bandari mpya ili kuongeza uwezo.

Mbossa alisema hayo mjini Bagamoyo mkoani Pwani alipofungua kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari.

Alisema serikali kupitia TPA imekamilisha Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa Bandari Tanzania kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2022 hadi mwaka 2045.

Mbossa alisema pamoja na masuala mengine, mpango huo umetoa dira ya uendelezaji wa na bandari za Tanzania kuanzia mwaka 2022 hadi 2045 kwa lengo la kuziboresha ili kuendana na matarajio ya ongezeko la shehena katika kila bandari.

“Ili bandari zetu ziweze kuhudumia ongezeko hili la shehena na kufikia ufanisi unaotakiwa, serikali inatakiwa kuwekezs katika miundombinu, ununuzi wa mitambo, mifumo ya Uendeshaji wa bandari, kuboresha uendelezaji, usimamizi na uendeshaji wa bandari zetu,” alisema.

Mbossa alisema mpango umetoa mapendekezo kwa serikali iendelee na urekebishaji wa Bandari ya Dar es Salaam wa kutafuta waendashaji binafsi wawili kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza gati za makasha namba tano hadi saba na nane hadi 11 kwa ajili ya kuongeza ufanisi.

Habari Zifananazo

Back to top button