TPA yatumia bilioni 1.146/- kusaidia afya, elimu, dharura
ZAIDI ya Sh bilioni 1.146 zimetumiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, TPA, kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya wananchi ya elimu, afya na kwenye huduma za kijamii.
Katika fedha hizo, Sh milioni 400 zimeenda kwenye huduma za jamii, Sh milioni 400 kwa ajili ya sekta ya afya na Sh milioni 346 zimepelekwa katika sekta ya elimu.
Akizungumza na HabariLEO kuhusu maadhimisho ya Siku ya Bandari, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa TPA, Nicodemus Mushi alisema kwamba mwaka huu siku hiyo itakayoadhimishwa katikati ya mwezi ujao, itahitimishwa kitaifa Mkoa wa Mtwara kwa kazi mbalimbali zikiwemo uwasilishaji wa huduma kwa wenye mahitaji.
Alisema maboresho katika sera ya urejeshaji wa faida kwa jamii (CSR) yaliyofanyika mwaka huu, 2023, unawezesha mamlaka hiyo kutoa huduma zake kwa jamii katika maeneo yenye shida zaidi ya wale walio karibu na miradi ya bandari au bandari zenyewe kama sera ya awali ilivyokuwa ikielekeza.
“Kwa sasa tunaangalia andiko lenye mashiko, linaloeleza changamoto iliyopo na juhudi zilizofanywa na wananchi wenyewe kabla ya kuomba sapoti (msaada),” alisema Mushi akifafanua urejeshaji wa mwaka huu ambao sasa unafanyika kwa kuangalia juhudi za wananchi zilizolenga kutatua shida waliyokuwa nayo.
Alisema kwa mwaka huu wametoa fedha kwa ajili ya urekebishaji wa miundombinu na vifaatiba katika hospitali kadhaa za wilaya ikiwamo ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Kahama mkoani Shinyanga huku pia sekta ya elimu ikinufaika katika miundombinu na vitendea kazi kama kompyuta.
Mushi alisema kwamba maboresho ya sera ya urejeshaji wa faida kwa wananchi ya mwaka 2023 imefanya taasisi hiyo kuangalia mahitaji ya wananchi wote ambao wameanza kushughulikia tatizo walilokuwa nalo na wao wanaenda kumalizia.
Alisema kiwango cha urejeshaji wa faida kwa umma kimekuwa kikiongezeka toka mwaka 2020/21 ambapo kilitolewa Sh milioni 350 hadi milioni 900 kwa mwaka 2023.
“Kutokana na uhitaji msaada katika sekta ya afya na elimu kuongezeka, mchango wa taasisi ulitoka katika makadirio ya mwanzo ya Sh milioni 900 hadi Sh bilioni 1.146,” alisema Mushi na kuongeza kuwa changamoto nyingi walizosaidia wananchi kumaliza shida zao iwe katika hospitali na maji kumewafanya wananchi kuwa rafiki wa bandari na kulinda miundombinu iliyopo.
Alisema CSR ni kiungo muhimu kati ya TPA na jamii inayozunguka miradi ya bandari na nyenzo muhimu sana katika kuitangaza bandari na shughuli zake. Alitolea mfano kuwa ujenzi wa kituo cha Polisi Karema uliofanywa na taasisi hiyo, ulitumika kutangaza uwapo wa Bandari ya Karema.
Maadhimisho ya Siku ya Bandari Kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Mtwara Septemba 15 na 16, mwaka huu.