TPA yaweka wazi tarehe ya kuanza usimamizi wa ‘TICTS’

MAMLAKA ya Usimamizi Bandari nchini (TPA) imesema itachukua rasmi usimamizi wa eneo lilokuwa likiendeshwa na Kampuni Binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS) kuanzia Januari Mosi, 2023 hadi hapo serikali itakapo amua vinginevyo.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Juma Kijavara amewaambia wanahabari mjini Bagamoyo kuwa uamuzi huo unatokana na mkataba kati ya TPA na Ticts kuisha muda wake. 

“Hapa hatujavunja mkataba. Kilichofanyika ni kwamba mkataba umemalizika na sasa eneo hilo linarudi kwa mmliki,” amesema Kijavara. “Tunaamini huduma zitaendelea na zitakuwa bora zaidi kama ilivyokuwa awali.”

TPA imesema baada ya kuchukua usimamizi wa eneo hilo, Mamlaka zimefikia makubaliano pia kuhusu mitambo iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni ya TICTS. Makubaliano hayo pia yanahusisha kuchukua watumishi wote waliokuwa chini ya TICTS.

“Ajira za watumishi hao ziko salama wataendelea kulipwa kama walivyokuwa wakilipwa kinachobadilika ni usimamizi tu,” ameongeza Mhandisi Kijavara. 

Habarileo linafahamu kuwa mkataba kati ya TICTS na TPA ulimalizika Septemba mwaka huu hata hivyo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi aliongeza miezi mitatu ili kuruhusu majadiliano yaliyokuwa bado yakiendelea kati ya pande hizo mbili. 

Kwa mujibu wa Kijavara mkataba wa TICTS na TPA unaisha rasmi Disemba 31. 

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button