TPDC mguu sawa ulipaji fidia Mtwara

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), leo  limeanza kufanya mchakato wa mwisho wa kulipa fidia kwa wananchi 255, ambao sehemu ya ardhi yao imechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Ntorya kwenda Madimba mkoani Mtwara.

Meneja Utawala TPDC, Linus Kinyondo amesema kiasi cha shilingi milioni 437, kimeshatengwa tayari kulipa fidia kwa walengwa.

“Zoezi tulilokuja kufanya sasa ni kukamilisha ulipaji wa fidia ya eneo ambalo bomba la gesi litapita, ” amesema.

Kinyondo amesema kabla ya ulipaji wa fidia hiyo walengwa watapewa elimu juu ya fedha na baadae kufunguliwa akaunti maalumu, ambazo watawekewa fedha yao ya fidia.

“Baada ya zoezi la kufungua akaunti, kutakuwepo na usainishaji wa mikataba, kila mguswa (mlengwa) atasaini mkataba na TPDC kuhusiana na malipo hayo,” amesema.

Kinyondo amesema kuwa kabla ya kuwekewa malipo yao kwenye akaunti, kila mhusika atasomewa kila kitu kilichopo kwenye mkataba ikiwepo stahiki zake na baadae malipo kufanyika.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Hanafi Msabaha amewaomba wananchi walengwa kutoa ushirikiano kwa wataalamu ambao wanahusika na fidia.

Habari Zifananazo

Back to top button