TPDC waanza utekelezaji bomba la gesi Mtwara

TPDC waanza utekelezaji bomba la gesi Mtwara

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), limeanza kutekeleza hatua za  kuanza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia, lenye urefu wa kilomita 35 kutoka eneo la Ntorya, Kata ya Nanguruwe kwenda kiwandani Madimba, mkoani Mtwara.

Hatua hizo zimeanza kutekelezwa na TPDC kwa kufanya tathmini ya mali,  ikiwemo ardhi katika njia inayotarajiwa kutumika kujenga bomba hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dustan Kyobya amezindua mradi  wa kufanya tathmini hiyo, huku akiitaka TPDC kushirikisha kikamilifu wananchi, wenyeviti na watendaji wa maeneo ambayo yatahusika katika ujenzi wa bomba hilo.

Advertisement

“Niwaombe TPDC mtoe ratiba kwa wenyeviti wa vijiji na watendaji wote kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika hatua zote zinazohusisha ujenzi wa bomba hilo,” amesema.

Kyobya amesema mradi wa ujenzi wa bomba hilo utaleta faida mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo ajira wakati wa ujenzi na uendeshaji wa bomba, fursa za kazi za usafi, huduma za vyakula na huduma za ulinzi.

Meneja wa biashara ya Gesi Asilia TPDC, Emmanuel Gilbert,  amesema shirika hilo linafanya tathmini ya mali kwenye njia ambayo inatarajiwa kutandikwa bomba hilo na kuanisha thamani, ili wananchi wanaomiliki mali hiyo waweze kulipwa.

“Kazi ya ujenzi wa bomba ni ya kutoa ardhi , na ardhi hiyo sio ya TPDC, kwa kutekeleza mradi huo, inahitajika ardhi ambayo inamilikiwa na wananchi,” amesema na kuongeza kuwa mali hiyo itafanyiwa tathmini na kuanishwa, ambapo thamani yake itajulikana, ili wahusika waweze kulipwa stahiki zao.