SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Nchi (TPDC) limeanza mchakato wa kuzalisha gesi asilia katika eneo la Ntorya lilipo katika kata ya Nanguruwe Mkoani Mtwara.
Mkurungenzi Mkuu wa TPDC, Dk. James Mataragio amesema wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurungezi kuwa uzalishaji wa gesi utaanza baada ya miezi 18 kuanzia sasa ambapo kiasi cha futi za ujazo milioni 60 zitakuwa zinazalishwa kwa siku. Gesi hiyo iligundulika mwaka 2012.
“Baada ya kuwa tumeanza uzalishaji wa awali wa futi za ujazo milioni 60 kwa siku tunategemea kwenda mpaka futi za ujazo milioni 140 kwa siku kwa miaka miwili inayo kuja,” amesema.
Amesema kwa Sasa Shirika lipo katika mazungumzo kampuni uchimbaji ya ARA (ARA Petroleum Tanzania Limited) ambayo itahusika katika shughuli za Uzalishaji wa gesi hiyo.
” Kwa Sasa tupo Katika hatua za kuanza kujenga bomba ambalo litakuwa na kilomita 35 kutoka eneo la Ntorya kwenda Kiwanda Cha kuchakata gesi Cha Madimba Mkoani Mtwara,” amesema.
Amesema shughuli za kujenga bomba zimeshaanza shughuli na kwamba wako katika hatua ya kuongea na Taasisi za fedha kujenga hiilo Bomba.
“Tumeanza kufanya upembuzi yakinifu kujua gharama za kujenga bomba zitakuwa kiasi gani,” amesema.
Ametaja baadhi ya shughuli ambazo zitahusika katika kujenga bomba hilo kuwa ni kujua eneo ambalo bomba litapita kujua gharama ya kulipa watu ambao wana mashamba na nyumba katika maeneo ambayo bomba litapita .