TPDC yachangia Tsh bilioni 295/-mfuko wa mafuta na gesi

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limechangia kwenye Mfuko wa Mafuta na Gesi kiasi cha Sh bilioni 295.55 kwa kipindi cha mwaka 2016 /2017 hadi kufikia Mei , 2022.

Ofisa wa TPDC wa Idara ya Biashara za Mafuta na Gesi , Mhandisi Eva Swillah amesema hayo Desemba 14, 2022 mjini Morogoro wakati wawasilisho la gesi asilia ,miradi na fursa zilizopo katika mkondo wa kati na wa chini wa petroli.

Shirika hilo liliandaa semina kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Morogoro iliyolenga kuwajengea uwezo wa kuandika na kutoa taarifa sahihi zinazohusu sekta ya mafuta na gesi asilia.

Mhandisi Swillah amesema licha ya kuchangia kwenye Mfuko huo ,TPDC imetoa gawio kwa serikali jumla ya Sh bilioni 9.34 kwa mwaka 2018/2019- 2021/22.

Amesema mchango wa gesi asilia katika uchumi ni mkubwa kwani fedha zilizookolewa kwa kutumia gesi asilia badala ya nishati mbadala kuanzia Julai , 2004 hadi Mei ,2022 zinafikia takribani Sh trillioni 41.13.

“ Mchango huo ni pamoja na kuongezeka uwekeaji wa kigeni nchini, wataalamu wa ndani ya nchi na katika sekta ya mafuta na Gesi asilia” amesema Mhandisi Swillah

Naye Gastony Canuty amesema TPDC inaendelea na shughuli za utafutaji , uzalishaji , uchakataji , usambazaji wa gesi asilia, uhifadhi na biashara ya mafuta ili kuhakikisha uwepo wa nishati ya kutosha nchini.

Canuty ambaye ni Ofisa kutoka Idara ya Mkondo wa Juu amesema mpaka sasa kiasi cha gesi asilia kilichogundulika ni futi za ujazo trillioni 57.54 ambapo zimejumuishwa za nchi kavu trillioni 10.41 pamoja na baharini trillioni 47.13.

Amesema sehemu ya kiasi hicho kinatumika katika miradi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme ambapo zaidi ya asilimia 70 ya umeme unaozalishwa katika gridi ya Taifa unatokana na gesi asilia na kuendeshea mitambo viwandani .

“ Kwa nchi kavu tumegundua eneo la Songo Songo, Mnazi Bay , Mkuranga , Ruvuma eneo la Ntorya pamoja na Ruvu , na gesi asilia inayotumia ni ile ya Songo Songo na Mnazi Bay “ amesema Canuty

Canuty amesema kwa sasa mikataba ya uzalishaji na ugawanaji inayofanya kazi ipo 11 , mitano ni ya utafutaji nchi kavu, mitatu utafutaji katika kina kirefu cha bahari na mitatu ni ya uendelezaji .

Hivyo ametaja vitalu vitano vina leseni za utafutaji maeneo ya nchi kavu na kampuni zake kwenye mabano ni Ruvu (DODSAL ), Ruvuma (ARA), Kilosa – Kilombero (SWALA) ,Tanga (AFREN) na Nyuni (Ndovu Resources).

Amesema vitatu vingine vina leseni ya utafutaji kina kirefu baharini na kampuni zake katika mabano ni kitalu namna 1 & 4 (SHELL, Ophir, na Pavillion Energy), kilatu namba 2 ( Equinor Exxonmobil).

Pia vingine vitatu vina mikataba yenye leseni ya uendelezaji nchi kavu na kampuni zake kwenye mabano ni Songo Songo (PAET), Kiliwani North ( Ndovu Resources), na Mnazi Bay ( Maurel & Prom).

Canuty amesema kazi inayoendelea katika kitalu cha Ruvu ni uchakataji na utafsiri wa data za mitetemo za 3D kilometa za mraba 481 umekamilika na maandalizi ya uchorogaji wa visima viwili kwa sasa unaendelea.

Kwa upande wa kitalu cha Ruvuma eneo la Ntorya amesema ,kazi inayoendelea ni ukusanyaji wa data za mitetemo za 3D ambayo imekamilika.

Canuty amesema kunafanyika maandalizi ya uchimbaji wa kisima kimoja pamoja na maadalizi ya kuunganisha eneo la Ntorya na Madimba, na kwa kitalu cha Kilosa- Kilombero kazi inayoendelea ni maandalizi ya uchimbaji kisima .

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Morogoro , Pascal Kihanga ,kwenye hotuba ya ufunguzi amewaomba waandishi wa habari wa mkoa huo kutumia uwezo waliojengewa na Shirika hilo kuyasemea mazuri yanayofanywa serikali ya awamu ya sita ya kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wake.

Habari Zifananazo

Back to top button