TRA Geita yatoa onyo biashara za magendo

GEITA; MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Geita imewataka wafanyabiashara kuachana na biashara za magendo badala yake kama wana dukuduku wafike ofisi za TRA ili kupatiwa elimu thabiti.

Ofisa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano ofisi za TRA Geita, Makilo Seuta amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Maonyesho ya Fahari ya Geita mjini.

Makilo amesema TRA inafanya kazi kwa urafiki na inatoa elimu ya huduma zote za kodi kwa kila mtu na hivo hakuna haja ya kuendesha biashara bila kulipa kodi kwani tabia hiyo inaminya mapato kwa taifa.

“Tunaendelea kuwakumbusha wafanyabiashara wetu, kwamba kodi zetu ndio zinaleta maendeleo katika nchi yetu.

“Waachane na biashara ya magendo, na biashara ambazo wanazifanya wahakikishe kwamba ni halali na zinaingizwa nchini kwa kufuata taratibu zilizopo.”

Makilo amesema pia wamewekeza katika elimu ya Mashine za Kutoa Risiti za Kielektroniki (EFD) ambapo ili kuongeza mwitikio wanashirikiana na wakala wa mashine za EFD kuwafikia wateja.

Ameongeza pia TRA mkoani Geita inaendelea kutoa namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN Number) kwa mfanyabiashara au mtu binafsi pamoja na Control number ili kurahisisha malipo ya kodi.

Habari Zifananazo

Back to top button