TRA Katavi wasikia kilio Kata ya Majimoto

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Katavi, imezindua ofisi ya kituo cha  huduma Majimoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, lengo likiwa kuwapunguzia adha walipa kodi ya kutembea umbali wa zaidi ya Kilometa 130 kufuata huduma.

Meneja wa TRA Mkoa wa Katavi, Jacob Mtemang’ombe, amesema awali walipa kodi wa Kata ya Majimoto, wapatao 550 walilazimika kutembea umbali huo, jambo lililokuwa likiwakatisha tamaa na wakati mwingine kukwepa kulipa kodi.

“Eneo hili tulilopo lina wafanyabiashara 550, ambao wameandikishwa katika mfumo wa mamlaka, hatua hii ya kufungua ofisi ya kutoa huduma ya kodi kutapunguza gharama za ulipaji kodi.

“Tunaamini ofisi hii ya huduma za kodi hapa Majimoto itaongeza ufanisi wa biashara na ukuaji wa uchumi kwa Halmashauri ya Mpimbwe na Mkoa kwa ujumla, kwani huduma za kodi zinapatikana kwa gharama nafuu na kwa wakati,” alisema Mtemang’ombe.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mlele, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ya uzinduzi, Lincolin Tamba, aliipongeza TRA kwa kusogeza huduma karibu, kwani itachochea mwamko wa wananchi kulipa kodi kwa wakati.

Amewasihi wafanyabiashara na wananchi wote kushirikiana na serikali kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali, kwa kuhakikisha muuzaji anatoa risiti na mnunuaji anadai risiti, huku akiwahimiza kutoa taarifa za matumizi yasiyo sahihi ya mashine za EFD na wakwepa kodi kwa kuendekeza vitendo vya rushwa.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kata ya Majimoto, Samwel Zablon, amewaomba maafisa wa TRA waliopewa dhamana ya kusimamia ofisi hiyo, wawe rafiki wa wafanyabiashara kwa kuwaelimisha badala ya kukimbizana.

Habari Zifananazo

Back to top button