TRA Kigoma yahamasisha umuhimu wa risiti

Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kigoma, imeeleza licha ya utoaji wa elimu ya mlipa kodi bado suala hilo limeendelea kuwa kikwazo katika mpango wa mamlaka hiyo kufikia malengo ya ukusanyaji kodi iliyojiwekea  hasa maeneo ya vijijini kwenye  shughuli za  kilimo.

Meneja wa TRA mkoani humo,  Deogratius Shuma alisema hayo katika kampeni ya TUWAJIBIKE iliyolenga kutoa elimu kwa wafanyabiashara kutoa risiti kila wanapouza bidhaa au kudai risiti wanaponunua bidhaa.

Shuma alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la wafanyabiashara wanaotoa risiti hasa kwa kutumia mashine za kielektroniki, lakini idadi inayotekeleza jambo hilo haiendi sambamba na idadi ya biashara ambazo zinatambulika.

Meneja huyo wa TRA Mkoa Kigoma alisema kuwa pamoja na changamoto hiyo wataendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao, hasa wa mazao vijijini ambao wamekuwa na mauzo makubwa yanayopaswa kutumia mashine na kutoa risiti.

Akieleza faida za utoaji risiti kwa wafanyabiashara Meneja huyo wa TRA alisema kuwa inawarahisishia wafanyabiashara kufanya makadirio ya kodi wakiwa na uhakika wa ukubwa wa biashara wanayofanya, hivyo kuondoa changamoto ya kukadiriwa kodi na maofisa wa mamlaka hiyo na kuanza kulalamika kubambikiwa kodi kubwa.

Awali maofisa wa TRA wakiwa katika shule ya Msingi Shabbir Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mkuu wa shule hiyo, Starkish Nyaga alisema kuwa wamekuwa wakipata changamoto kubwa wanapokwenda vijijini kununua mazao kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa shule hiyo, lakini hawapati risiti kutoka kwa wauzaji hao.

Akizungumza katika kampeni hiyo Katibu Tawala Msaidizi seksheni ya uchumi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Mtime Mwalyambi amewataka wafanyabiashara kuunga mkono juhudi za serikali kupitia TRA katika ukusanyaji wa mpato kwa kutumia mashine za EFD.

Mwalyambi alisema kuwa ukusanyaji mapato kutumia mashine za EFD unaiwezesha TRA kukusanya kodi ya kutosha na hivyo kuiwezesha serikali kuwa na mapato ya kutosha kugharamua shughuli za maendeleo kwa wananchi wake.

Kampeni ya TUWAJIBIKE ilizinduliwa na kuanza Machi 2 mwaka huu, ikiwa na malengo ya kutoa risiti halali, kudai risiti halali na kuchukua hatua kwa wauzaji wasiotoa risiti halali za EFD.

 

Habari Zifananazo

Back to top button