TRA wakamata bidhaa za magendo Kigoma

KIGOMA: MAMLAKA ya Mapato mkoani Kigoma imekamata bidhaa mbalimbali za vinywaji vya kuongeza nguvu na vipodozi vikiingizwa nchini kwa kutumia njia za panya ili kukwepa kulipa kodi.

Meneja wa TRA mkoani Kigoma, Deogratius Shuma akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwenye kituo cha forodha cha mamlaka hiyo eneo la Manyovu Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma amesema bidhaa hizo ambazo thamani yake haijulikani ziliingizwa kupitia vijiji vilivyopo mpakani mwa Tanzania na Burundi katika Wilaya ya Buhigwe.

Alivitaja bidhaa hizo kuwa  ni pombe kali aina ya Karibu Waragi Gin katoni 95, Dubai Gin katoni tano,kinywaji cha kuongeza nguvu aina ya akayabagu katoni  nane, vipodozi vilivyopigwa marufuku katoni 106.

Advertisement

Katika operesheni hiyo pia wamekamata  mifuko 15 ya vipodozi ya kilo 25 kila moja aina ya Altar Marine Blue ambavyo pia vinatumika kama kemikali ya kutengenezea sabuni na sigara aina ya club ambazo zimeingizwa bila kufuata taratibu zakulipiwa ushuru.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Buhigwe wakiongea na waandishi wa habari wamesema kuwa uingizaji bidhaa kwa njia ya magendo kuna athari kwa nchi kwani unaifanya serikali kushindwa kukusanya mapato ya kutosha ambayo ndiyo yanayosaidia kugharamia miradi ya wananchi.