TRA yaja kivingine ukusanyaji mapato

HALMASHAURI ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro imeanza kazi ya kuwatambua wafanyabiashara wake wote ili wasajiliwe kwenye mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, David Mgonja ameeleza hayo alipozungumza na HabariLeo.

Amesema Julai mosi mwaka huu ndio kazi hiyo ilianza ambapo timu ya maofisa biashara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliwatembelea wafanyabiashara hao.

Amesema hilo linafanyika ili ukusanyaji mapato kupitia leseni za biashara uweze kurahisishwa.

” Tumefanikiwa kuwafikia wafanyabiashara katika kata za Kindi, Mabogini, Kate Magharibi na Uru Kusini.

” Kazi ya kuwafikia wafanyabiashara katika vijiji na kata itaendelea na sasa timu ya maofisa biashara wanahamia Kata ya Arusha chini na baadaye kata zilizobakia,” amesema.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Mkurugenzi iliandaa mafunzo kwa watendaji wa vijiji na kata zote Septemba 21 na 22 mwaka huu ili kuwajengea uwezo namna ya kuwasajili wafanyabiashara kwenye mfumo ujulikanao kama tausi katika maeneo yao.

Amesema changamoto iliyopo ni kwa baadhi ya wafanyabiashara kutojitokeza kwenye usajili na mafunzo katka kambi zinazowekwa kwenye vijiji na kata.

Halmashauri hiyo ina kata 32 na vijiji 157, inawafanyabiashara takribani 4800.

Habari Zifananazo

Back to top button