MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imejidhatiti kuondoa makadirio ya kodi yanayodaiwa kuwa kandamizi kwa wafanyabiashara ili kufikia adhma ya kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari.
Ofisa Msimamizi Mwandamizi wa Kodi Idara ya Elimu na Mawasiliano kutoka TRA Makao Makuu, Isihaka Shariff alisema hayo wakati wa utoaji elimu kwa mlipa kodi katika Mamlaka ya mji mdogo Katoro wilayani Geita.
Amesema katika kipindi hiki cha makadirio ya kodi ambacho hufanyika miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka (Januari hadi Machi) TRA imekuja na kampeni ya kupita mlango kwa mlango kutoa elimu ya kodi.
“Tunawafikia wafanyabiashara wote wanaopasawa kurasimisha biashara zao ndio maana tumekuja na zoezi la mlango kwa mlango, hutuachi mtu, tunapita kila eno na kila biashara ya duka kwa duka.” Ameeleza.
Amesema ili kupunguza malalamiko ya makadirio ya kodi, TRA imetoa nafasi kwa wafanyabiashara wanapokumbana na mabadiliko kwenye biashara zao kufika TRA kurekebisha makadirio yao.
“Kama biashara ikiyumba, lakini pia biashara ikiongezeka unawezesha kurekebishiwa makadirio, kwa maana biashara inaweza ikaenda chini au ikapanda juu, utakadiliwa kwa uhalisia wa biashara yako.” Amesema.
Amesema, timu ya TRA inazunguka kwenye maeneo tofauti kutoa elimu ya kodi, kufanya ukaguzi wa biashara na kuona na kutatua changamoto zao na kuwakumbusha waende kufanya makadirio ya kodi.
Amesema walichobaini pia bado kuna baadhi ya wwafanyabiashara hawana ya kutoa Risiti za Kielektroniki (EFD) na wengine wana mashine za EFD lakini bado wanapata changamoto kwenye kutumia.
“Tunawaelimisha namna bora ya kuweza kutumia hizo mashine. Hii inasaidia kwa sababu lengo kubwa la mamlaka kwanza ni kukusanya lakini pili kumfanya kila mtu awe mzalendo.” Amesema.
Mmoja wa wafanyabishara katika Mamlaka ya mji Mdogo wa Katoro, John Elias amekiri elimu ya TRA ya mlango kwa mlango imewaondolea dhana potofu kuhusu suala la makadirio ya kodi kutoka TRA.