TRA Katavi yakusanya zaidi ya bilioni 7/-
Katika mwaka wa fedha 2021/22 Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Katavi imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 7.2 sawa na ufanisi wa asilimia 117.42 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 6.2.
Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwatunuku vyeti washindi wa tunzo ya mlipa kodi bora wa mwaka 2021/22, Kamishna Mpelelezi wa Kodi TRA Makao Makuu, Andengenye Mwaipopo amesema makusanyo hayo ni ongezeko la Tsh. Bilioni 1.7 ikilinganishwa na kiwango cha makusanyo ya bilioni 5.
4 kilichofikiwa mwaka 2020/21.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Jamila Yusuf kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Katavi ameipongeza Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Katavi kwa kuvuka lengo huku akitoa wito kuhakikisha mafanikio hayo yanaamsha ari ya kufanya vizuri msimu ujao na si kubweteka.
Jamila amesema ipo tabia ya baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitoa risiti ziziso sahihi na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja kwani ni kosa kisheria.
“Nichukue furasa hii kuiagiza TRA kuwa wakali kwa maana utoaji wa risiti za EFD ndiyo msingi wa kukadiria kodi kwa haki bila kumuonea mtu yoyote na bila kuipunja serikali”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara tawi la Katavi, Amani Mahela amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa TRA na kuhakikisha wanakuwa waaminifu kwa kulipa kodi stahiki kwa wakati kwa mstakabali wa Taifa.