TRA yakusanya Sh Tril. 5.9 miezi mitatu

MAMLAKA ya Mapato Tanzania ‘TRA’ imesema imefanikiwa kukusanya Sh trilioni 5.9 ambazo sawa na asilimia 97.9 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 6.0, katika kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023. Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 6.1 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2021/2022.

Taarifa iliyotolewa leo Aprili 4, 2023 na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata imeeleza kuwa makusanyo hayo yamechangiwa na uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji kodi ambayo imerahisisha utaratibu wa ulipaji kodi kwa hiari pamoja na kuongezeka kwa uwezo wa walipakodi katika kulipa malimbikizo ya kodi.

Advertisement

Katika taarifa hiyo imeeleza sababu nyingine kuwa ni kuimarika kwa mahusiano baina ya mamlaka na walipakodi ikiwemo utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya mahakama pamoja na kushughulikia malalamiko ya walipakodi kwa wakati.

Sambamba na hilo TRA imeeleza sababu nyingine kuwa ni kujengeka kwa imani kwa wafanyabiashara kufuatiwa uwezeshaji wa mazingira mazuri ya kufanyia biashara.

TRA imewataka wafanyabiashara wote na taasisi za serikali zikiwemo halmashauri kuzingatia matumizi sahihi ya risiti za kielektroniki za ‘EFD’ na kwamba ni wajibu wa kila mwananchi anapopata huduma au kununua bidhaa kudai risiti.