MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na serikali kwa taasisi hiyo kukusanya mapato ya Sh trilioni 24.11 kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata kwa vyombo vya habari jana, kiasi hicho ni sawa na asilimia 97.4 ya lengo.
“Lengo lilikuwa kukusanya Sh trilioni 24.76… makusanyo haya ni sawa na ongezeko la asilimia 8.2 ikilinganishwa na kipindi kilichopita cha mwaka 2021/22,” alieleza Kidata.
Aliongeza: “TRA inaendelea kumshukuru Rais Samia na serikali yake kuendelea kuwezesha katika utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kiutendaji.” Aidha, alisema TRA inatoa pongezi za dhati kwa walipa kodi na wadau mbalimbali kwa kuiwezesha kufikia hatua hiyo.
“Mamlaka inapenda kutoa rai kwa wananchi wote kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhimiza ulipaji wa kodi stahiki na mahususi katika kusisitiza juu ya ulipaji kodi kwa hiari,” alisema.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/24, TRA imetoa rai kwa walipa kodi na wananchi kwa ujumla kuzingatia maelekezo yao.
“Wauzaji wote wa bidhaa na huduma mbalimbali wahakikishe wanatoa risiti sahihi za kielektroniki (EFDs) katika kila mauzo wanayofanya na kwamba wanunuzi wote wadai risiti sahihi za kielektroniki katika kila bidhaa au huduma,” alisema.
Alisema walipa kodi wanatakiwa kuwasilisha ritani sahihi, kulipa kodi stahiki na kulipa madeni ya kodi kwa hiari na wakati uliowekwa kisheria ili kuepukana na riba na adhabu zisizo za lazima.
“Wazalishaji na waingizaji bidhaa nchini zinazotozwa ushuru wa bidhaa na walipa kodi na wadau wetu kuendelea kuhudhuria mafunzo mbalimbali yanayotolewa na mamlaka juu ya elimu ya kodi na matumizi ya mifumo ya usimamizi wa kodi ili kupata elimu inayowajengea uwezo kwenye masuala yanayohusu kodi na usimamizi,” alisema.