MAMLAKA ya Mapato (TRA) Mkoa wa Katavi, imetangaza kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara watakaobainika kufanya udanganyifu kwa kutoa risiti za uongo kwa wateja wao kwa lengo la kukwepa kulipa kodi.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TRA mkoa huo Jacob Mtemang’ombe, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake akitambulisha kampeni ya Tuwajibike kwa Mkoa wa Katavi.
Mtemang’ombe amesema mpaka sasa tayari wafanyabiashara watano wamechukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kufikishwa mahakamani kutokana na kutoa risiti za uongo kwa wateja.
“Kuna malalamiko mengi sana tumepata kutoka kwa wanunuzi, wananunua kitu cha shilingi 20,000 wanapewa risiti ya shilingi 2,000 na watu wengi hawaoni umuhimu wa kuangalia hizo risiti wanaponunua bidhaa, hivyo wafanyabiashara hutumia nafasi hiyo kupunguza bei katika risiti hizo.
“Risiti halali inatakiwa ioneshe uliponunua bidhaa, jina lako, tarehe, muda, kiasi cha bidhaa ulionunua, namba yako ya TIN ingawa kuna wengine hawana TIN lakini hivi vigezo ukiangalia kama vimekamilika basi risiti hiyo ni sahihi,” amesema Mtemang’ombe.
Aidha Mtemang’ombe ametoa wito kwa wananchi kudai risiti huku akisema mnunuzi yeyote asiyedai risiti anachukuliwa hatua ya kutozwa faini kuanzia Sh 30,000, hadi shilingi milioni 1.5 kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa kodi.
Amesema kampeni ya Tuwajibike inahusisha wananchi wote na imekuja kwa lengo la kuikumbusha jamii kuwa kila mmoja ana wajibu wa kufanya kile ambacho anapaswa kufanya.
Amesema wamekuja na kampeni ya Tuwajibike kutokana na matumizi ya mashine za Kielektroniki kupungua hasa kwa wafanyabiashara na sekta mbalimbali zinazojihusisha na biashara, hivyo kampeni hiyo itasaidia kuwakumbusha kuendelea kutumia mashine hizo.