MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), Mkoa wa kikodi Kahama, imewataka wafanyabiashara kuacha kuwatumia wahasibu vishoka, ambao wamekuwa wakiwasababishia mtafaruku kwa kupewa madai makubwa ya kodi katika biashara zao.
Hayo yamesemwa leo Agosti 22, 2022 na Meneja Msaidizi wa Ukaguzi wa Hesabu kutoka mamalaka hiyo, Honest Mushi, akimwakilisha Meneja wa Mkoa, Warioba Kanile kwenye semina ya wafanyabiashara, iliyolenga kutoa elimu juu ya mabadiliko ya kodi kulingana na sheria ya fedha ya mwaka 2022.
“Kuna wahasibu vishoka hasa kwenye mikoa midogo, hilo tunalijua sababu wahasibu wa kupiga hesabu tunawasajili sisi, lakini ninyi wafanyabiashara mmekuwa mkiwatumia vishoka, ambao hawajui hesabu, wanachotaka kuwalia hela zenu,” amesema Mushi.
Mushi amesema kuwa kulipa kodi ni suala la msingi, lipangiwe bajeti mahususi ndani ya biashara, pia mfanyabiashara anatakiwa awe na wahasibu wa kumpigia hesabu kwa ajili ya kulipa kodi kabla ya kufika TRA.