MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kigoma, imekabidhi misaada mbalimbali ikiwemo magodoro 32 ya kulalia kwa gereza la kilimo la Ilagala wilayani Uvinza mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukurani kwa jamii ikiwa ni kuanza kwa mwaka mpya wa fedha 2022/23 wa kiserikali.
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo kwa uongozi wa gereza la Ilagala, Meneja wa TRA Mkoa Kigoma, Deogratius Shuma alisema msaada huo una thamani zaidi ya shilingi milioni mbili na wanaamini misaada hiyo itaenda kuongezea pale palipokuwa pamepungua, ili wafungwa waweze kupata mafunzo yao ya kila siku wakiwa vizuri.
Shuma alisema msaada huo unatokana na watumishi kujichangisha wenyewe na ofisi iliweza kutoa kiasi kidogo kuongezea na kuweza kununua vitu hivyo, ambavyo wanaamini itakuwa msaada kwa wahitaji ingawa inaweza isimalize tatizo la mahitaji walilonalo wafungwa hao.
Alisema kilichowasukuma zaidi kwenda kutoa msaada huo katika gereza hilo ni tukio la kupewa msaada na wafungwa hao wakati wakitimiza majukumu yao baada ya kukamata mzigo wa vitenge vya magendo eneo la ziwani karibu na gereza hilo.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa gereza la Ilagala, Nicholaus Kubyulwa ameshukuru kwa kupata msaada huo akieleza kuwa utatumika kwa ajili ya walengwa, kwani wangeweza pia kupeleka sehemu nyingine lakini wametambua mchango wao na ndio maana wakaamua kupeleka gereza hilo.
Mkuu huyo wa gereza alisema kuwa magereza ni eneo la kumrekebisha mtu na si kumkomoa mtu hivyo ana haki ya kupata mahitaji muhimu kama mtu mwingine ili akiwa katika mafunzo yake ya kurekebishwa aweze kufanya vizuri na hatimaye kubadilika na kuwa raia mwema.
Comments are closed.