TRA yapunguza tozo ya vitenge

lengo ni kupunguza magendo

SIKU chache baada ya Mtandao wa HabariLeo kuandika kuhusu njia zinazotumika kuhusiana na magendo hususani vitenge na vipodozi katika bandari bubu za Dar es Salaam na malori ya mafuta, hatimae Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeondoa  kodi hivyo kutoa unafuu kwa wafanyabiashara

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Richard Kayombo amesema hayo wakati Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alipotembelea mamlaka hiyo katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Mbeya.

Kayombo amesema upunguzwaji huo wa kodi kwenye vitenge utaondoa magendo yaliyokuwa yakifanywa.

“Kwa miaka ya hivi karibuni tulikuwa kidogo na changamoto upande wa uletaji wa vitenge,  wafanyabiashara walikuwa wanatozwa kodi, hivyo imeondolewa,”amesema Kayombo na kuongeza

“Kwa mwaka huu wa fedha kodi katika uagizwaji wa vitenge ambayo inatumiwa na watu wengi na vingine vinazalishwa kwa wanaoagiza kodi imepunguzwa kwa kiwango  kikubwa, ili kuondoa magendo pia kuleta uwiano ulio sawa kwa wanaozalisha vitenge nchini,” amesema.

Kauli ya Kayombo imekuja ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu Mtandao huu wa HabariLeo kufanya uchanguzi na kubaini mabilioni ya fedha ambayo yamekuwa yakipotea kutokana na uingizaji wa bidhaa kwa njia ya magendo.

Amesema hivi karibuni bunge lilipitisha bajeti iliyotoa unafuu kwa wanaoagiza vitenge, kwani imepunguzwa kutoka asilimia 50 hadi 35, ili kuondoa usumbufu wa magendo katika mipaka, pamoja na kusababisha uhaba wa bidhaa hiyo.

Pia amesema wafanyabiashara waliopo kwenye sekta ya kilimo wanapouza bidhaa nje ya nchi hazitozwi kodi ya aina yoyote, isipokuwa korosho pamoja na ngozi ghafi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Kigahe amepongeza TRA kwa jitihada za ukusanyaji kodi inayofanya na kwamba hivi sasa wananchi wangependa kujua baadhi ya misamaha na mabadiliko mbalimbali ya kikodi.

“Suala la vitenge limekuwa ni kero kwa muda mwingi hapa lazima tujue lengo la serikali ni kuhamasisha uwekezaji nchini,” amesema.

“Nashukuru TRA  na Wizara ya Fedha tumejadiliana angalau tupunguze kidogo ile kodi waliyokuwa wanatozwa waingizaji wa vitenge na kanga kutoka nje,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button