TRA yataka kukusanya Sh bilioni 69

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Morogoro imewekewa lengo la kukusanya Sh bilioni 69.63 kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 na katika kipindi cha miezi mwili Julai na Agosti imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 9.32

Kaimu Meneja wa TRA mkoa huo, Chacha Gotora alisema hayo alipomkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima kufungua kikao cha wadau wa sekta mbalimbali za uchumi wa mkoa huo kwa lengo la kutatua changamoto za wadau hao katika kulipa kodi.

“ Hiki kikao cha kawaida, TRA ina wajibu wa kukutana na wadau wake kwa lengo la kuwaelimishaa masuala ya kodi na kujadiliana ili kufikia makubaliano juu ya masuala mbalimbali ya msingi” alisema Chacha

Advertisement

Chacha ambaye ni Meneja Msaidizi – Huduma kwa Walipakodi wa Mamlaka hiyo mkoa alisema lengo la miezi miwili hiyo ilikuwa  ni kukusanya mapato ya Sh bilioni 10.38 .

Lakini kwenye makusanyo halisi  katika kipindi hicho  zilikusanywa Sh bilioni 9.32 ambalo ni sawa na mafanikio ya utendaji wa kazi zaidi ya asilimia 89.81

Chaha alisema  lengo la makusanyo ya kodi za ndani kwa miezi hiyo  lilikuwa zaidi ya Sh bilioni 10  lakini makusanyo halisi ni Sh bilioni 9.114 wakati kodi za forodha lengo lilikuwa ni Sh milioni 180 lakini makusanyo halisi ni Sh milioni 209

Alisema ili kufanikisha lengo la serikali kwa mwaka huu, TRA imedhamiria kuimarisha usimamizi wa utoaji wa risiti hasa risiti za kieletroniki , kukusanyaa malimbikizo ya madeni ya kodi.

Chacha alijataa eneo lingine ni kuwatembelea wafanyabiashara mara kwa mara ili kutenda haki katika ukadiriaji  na ukusanyaji wa kodi, kushirikiana na wadau katika kuibua vyanzo vipya vya mapato na majukumu mengineyo ili kuongeza ufanisi wa kazi .

Malima kwenye  hotuba yake ya ufunguzi  aliuagiza uongozi wa TRA mkoa na Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani humo kutoa elimu kwa wafanyabiashara itakayotoa matokeo chanya katika kuongeza ukusanyaji wa kodi.

“Elimu iwe jumuishi kwa ajili ya kuweza  kuwafikia wananchi kwa maana ya wafanyabiashara wa makundi yote ndio wanaoendesha uchumi wa nchi.” alisema Malima

Mkuu wa mkoa pia aliwataka wafanyabiashara kuifanyia kazi elimu inayotolewa kwao na mamlaka hiyo ikiwemo elimu ya matumizi mashine ya EFD.

Alisema ,baadhi ya wafanyabiashara wameonekana hawatekelezi majukumu yao  ipasavyo na kufanya ukusanyaji wa mapato serikalini kuwa ya chini.

Mwenyekiti TCCIA Mkoa wa Morogoro,  Mwandhini Myanza pamoja na kuipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara, aliwasihi wafanyabiashara kuacha tabia ya udanganyifu kwa kutumia mfumo wa kielektroniki vibaya kwa kuwatolea wanunuaji wa bidhaa risiti zisizo na majina yao.

Pia kuacha udanganyifu wa kutoa risiti zenye kuonesha gharama tofauti za manunuzi jambo ambalo linakwenda kinyune na sheria za Kodi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *