MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewapa semina waandishi wa habari kuwajengea uwezo kuhusu masuala mbalimbali ya kodi.
Akizungumza wakati wa semina hiyo Chuo Cha Kodi kilichopo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema lengo ni kuwapa elimu wanahabari ili waende kutoa elimu kwa jamii kuhusu kulipa kodi.
Amesema elimu hiyo ni pamoja na kuongeza ujuzi na kufundisha uelewa wa kulipa kodi ambayo elimu hiyo haitofautiani sana na masuala ni yale ambayo kila siku unapozidi kujifunza unapata elimu zaidi, ikiwa ni lengo kujenga Taifa moja.
“Hivyo ni wajibu wa kila mlipa kodi kuandikishwa kwa ajili ya kodi pale ambapo sheria za kodi zinamtaka kufanya hivyo,pia ana wajibu wa kuwasilisha ritani na kufanya malipo ya kodi kwa wakati kama ulivyowekwa kwa mujibu wa sheria ya kodi,” amesema Kayombo.
Pia amesema mfanyabiashara ana wajibu wa kudhihirisha shughuli zake za kibiashara pamoja na matokeo yake kwa ukamilifu na kwa usahihi, wajibu wa kutoa risiti za kodi kila anapouza bidhaa au anapotoa huduma,na wajibu wa kudai risiti za kodi kila anaponunua bidhaa au anaponufaika na huduma iliyotolewa.