TRA yawafunda walimu Geita

MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA) mkoani Geita imewataka walimu kuwajibika kukata na kulipa kodi ya zuio katika miradi inayotekelezwa kwa  Force Akaunti ili ikamilishwe kwa matakwa ya kisheria.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Geita, Adam Mabeho ametoa maelekezo hayo katika semina maalum iliyowakutanisha takribani walimu wakuu 700 kutoka shule za msingi na sekondari wilayani Geita.

Amesema kwa siku za hivi karibuni walimu wakuu ndiyo wasimamizi wa miradi inayotekelezwa na serikali shuleni hivyo ni lazima wanapofanya malipo ya utekelezaji wa miradi wanatakiwa kukata kodi ya zuio.

Ofisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA mkoa Geita, Justine Katiti, akizungumza katika semina hiyo. (Picha zote na Yohana Shida)

Amesisitiza, ili kufanikisha utekelezaji wa sheria hiyo pia wanatakiwa kuzingatia utaratibu wa kusajili TIN kwa shule zao sambamba na kuambatanisha matumizi sahihi ya mfumo wa marejesho (returns).

“Tumewaita walimu hawa lengo ni kuhakikisha kodi ya zuio kutoka kwenye miradi ya serikali inalipwa kwa usahihi na inafika mamlaka ya mapato kwa mjibu wa sheria.

“Tumegundua kwamba  kwa kuwa walimu wana majukumu mengi na jambo hili limekuwa ni jipya kwao, tumeona umuhimu zaidi wa kuwa karibu nao, kuzungumuza nao, kuwapa elimu na kuwasilikiza,” amesema.

Ofisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA Mkoa Geita, Justine Katiti amewaomba walimu kuzingatia uwasilishaji wa kodi ya zuio kwa wakati mara baada ya kukata ili kuepuka ongezeko la riba lisilo la lazima.

“Sheria imeelekeza kwamba usipolipa kwa wakati maana yake itaongeza riba, sasa ile riba atakayaeilipa siyo yule ambaye umemkata, bali ni wewe ambaye umechelewa kuilipa.”

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Colnery Magembe, akizungumza katika mafunzo hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Colnery Magembe amewaomba walimu kuwa mabalozi wazuri wa TRA kwani kodi inayopatikana ndio chachu ya maboresho ya huduma za kijamii chini ya usimamizi wa serikali.

“Ni fedha hizo hizo zinazokusanywa na TRA ndiyo zinazotulipa mishahara, ni fedha hizohizo zinazokusanywa na TRA ndiyo zinatufanya tupate huduma ya matibabu ya hospitali na zahanati zetu,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button