TRA yawapa elimu ya kodi wafanyabiashara Kagera

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), mkoani Kagera imekutana na wafanyabiashara, ili kutoa elimu juu ya mabadiliko mbalimbali ya sheria za kodi kwa mwaka 2022/2023.

Ofisa Msaidizi wa Kodi anayesimamia utoaji wa elimu na huduma kwa mlipa kodi, Alex Mwambenja, aliwaambia wafanyabiashara kuwa ni vyema wakayatumia mabadiliko ya  sheria za kodi kukuza biashara wanazozifanya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,  ili kuwa washindani wazuri wa bidhaa wanazozizalisha.

Alisema bidhaa ambazo zimefanyiwa mabadiliko na kupewa msamaha ni bidhaa za mafuta yanayozalishwa nchini, bidhaa za vifungashio vya maziwa, mashine za kuongeza thamani katika bidhaa za ngozi.

Pia amesema vifungashio vya plasitiki ambavyo vinafunga mbogamboga na maua kwenda nje ya nchi havitalipa kodi, ili kuongeza ushindani wa kibiashara ndani na nje ya nchi na kupunguza mfumuko wa bei.

“Tunaona pia kuna bidhaa zimeongezewa kodi zaidi, mfano nywele bandia, kope, ndevu bandia, bidhaa zenye sukari kutoka nje ya nchi, vyuma vya shaba vinavyouzwa nje ya nchi hivyo vyote vimeongezewa kodi.

“Hivyo kama kuna mtu anafanya biashara katika maeneo ya kilimo, mifugo na uvuvi, sehemu kubwa wamepunguziwa mzigo na hii ni kutokana na maoni, ambayo mmekuwa mkiyatoa tunayawasilisha, ” alisema Mwambenja.

Pia mamlaka hiyo mkoani Kagera, ilitoa pongezi kwa serikali kwa kutoa ajira kwa watumishi wapya   wa TRA na kuuwezesha mkoa wa Kagera kupata watumishi 50, ambao wamewezesha usajili wa wafanyabiashara wapya zaidi ya 300, tangu walivyoajiriwa.

Nicholaus Basimarki, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera, alisema serikali imeendelea kuwapa nafasi wafanyabiashara, hivyo ni vyema wasikwepe majukumu yao ya kulipa kodi bali walipe kodi kwa usahihi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x