TRA yaweka mkakati ukusanyaji kodi Kariakoo
MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), imeweka mkakati wa kuchochea wafanyabiashara kulipa kodi, ili kuongeza mapato ya serikali kwa kuweka mabango kwenye maeneo mbalimbali ya wazi yenye kuonesha ujumbe mbalimbali wa kodi, ikiwemo kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za Kieletroniki za kutoa risiti (EFD).
Meneja wa Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Alex Katundu amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mabango hayo yanayoelekeza kutoa na kudai risiti za EFD, katika eneo la kibiashara la Kariakoo.
Amesema mkakati wa pili wa TRA ni kuwasajili wamachinga wote waliopo katika eneo la biashara Kariakoo, ikiwa ni pamoja na kununua mashine za kielektroniki za kutoa risiti.
Amesema mkakati huo ni kwa ajili ya kuboresha usimamizi wa kodi katika eneo hilo, ambalo ndio kitovu kikuu cha biashara nchini.
Amesema kazi ya kusajili wamachinga hao inaendelea nampaka sasa wemeshasajiliwa wafanyabiashara wadogo wapatao 5, 273 ndani ya Mkoa wa Kariakoo.
Pia amesema mkakati mwingine walionao ni kubandika stika zenye kuonesha TIN ya mwenye duka kwenye maduka ya wafanyabiashara wote waliopo Kariakoo, ili mteja aweze kuhakiki taarifa zilizopo kwenye risiti ya EFD aliyopewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Ng’wilabuzu Ludigija amesema Kariakoo ndio eneo la kitovu cha biashara nchini, ambalo ni eneo pekee linalokusanya wafanyabiashara ndani na nje ya nchi.
Amesema serikali inafanya jitihada mbalimbali, ili kuhakikisha biashara zinakuwa, ili wafanyabiashara waweze kulipa kodi.