KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema Mamlaka ya Mapato (TRA) imeshindwa kukusanya kiasi cha Shilingi trilioni 2.8 kwa mwaka wa fedha 2020/21 kutokana na sababu kadhaa ikiwemo kutoshughulikiwa kwa madeni na mashauri ya kikodi.
Akisoma taarifa ya Kamati hiyo bungeni Dodoma leo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga amesema kuwa Mamlaka hiyo iliweka makadirio ya kukusanya kiasi cha Sh trilioni 20.7 kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2021 lakini kiasi halisi kilichokusanywa Tanzania Bara na Zanzibar kilikuwa ni Sh trilioni 17.89 pekee.
Nakisi hiyo ni sawa na asilimia 14 ya makusanyo hayo, ripoti hiyo imebainisha.
“Nakisi hiyo imechangiwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoshughulikiwa ipasavyo kwa madeni ya kodi pamoja na uwepo wa mashauri ya kodi ambayo hayajatolewa uamuzi katika vyombo vya Sheria kama Mahakama, Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT),” Bunge limeelezwa.
Kwa upande mwingine, eneo jingine ambalo taarifa ya Kamati imefafanua kwa kina ni malipo ya kiasi cha Dola za Marekani Milioni 153.43 yaliyofanywa na TANESCO kwa Kampuni ya Symbion kutokana na kuvunjwa kwa mkataba.
“Taarifa imebainisha kuwa, hasara hii ambayo Serikali imeingia inatokana na mapungufu katika makubaliano yaliyofikiwa kati ya TANESCO na Symbion pamoja na kutofanyika kwa upembuzi wa kina kabla ya kuvunjwa kwa mkataba huu,” amesema.