SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) kati ya Julai mwaka 2020 hadi Julai Julai mwaka huu limekusanya zaidi ya Sh milioni 400 kwa abiria wanaosafiri kutoka Dar es Salaam hadi Arusha.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete pia alisema katika muda huo, TRC imesafirisha tani 11,600 za mizigo vikiwamo vifaa vya ujenzi hivyo kuwezesha kupungua bei za bidhaa za ujenzi katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Mwakibete aliwaeleza waandishi wa habari Arusha kuwa usafiri wa reli umerahisisha huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kwa wananchi na wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Alisema TRC imejipanga kuboresha huduma wakati wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya na kwamba, ifikapo Desemba 20 mwaka huu, serikali itakuwa imeingiza mabehewa ya kisasa kwa reli za Dar es Salaam hadi Arusha, Dar es Salaam hadi Kigoma na sehemu nyingine.
‘’Serikali ya awamu ya sita iko katika mstari wa mbele kuhakikisha reli ya mwendo wa kawaida na kasi zinafanya kazi, hivyo ni wajibu wananchi kuunga mkono jitihada hizo,’’alisema Mwakibete.
Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa TRC, Focus Sahani alisema shirika hilo limejipanga katika kipindi cha sikukuu za mwishoni wa mwaka kuhakikisha linatoa huduma za uhakika kwa wasafiri wanaokwenda na kutoka ukanda ya kaskazini.
Sahani alisema ikibidi TRC inaweza kuongeza siku ndani ya wiki katika kipindi hicho. Alisema mbali ya abiria, wamekuwa wakipokea mizigo mingi inayosafirishwa katika ukanda wa kaskazini na bei ya vifaa vya ujenzi zimekuwa zikishuka.